Watu kumi wameripotiwa kuuawa na wengine kujeruhiwa baada ya watu wenye silaha
kuvamia makanisa mawili katika mji wa Garissa, kaskazini mashariki mwa Kenya hii
leo.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Upelelezi nchini Kenya, Muhoro Ndegwa, watu waliouawa
saba ni raia na maafisa wawili wa polisi waliokuwa wakilinda maeneo ya ibada
katika kanisa la Africa Inland Church, AIC.
Kanisa jengine lililoshambuliwa ni Kanisa Katoliki ambapo magruneti mawili
yalirushwa, ambapo moja liliripuka na kujeruhi watu kadha.
Hakuna mtu wala kikundi kilichodai kuhusika na mashambulio hayo, japo katika
mashambulio kadhaa ya siku zilizopita yalihusishwa na wanamgambo wa Kiislam wa
Somalia wa kundi la Al-Shabaab.
Kenya ilipeleka vikosi vyake nchini Somalia mwaka jana kuwasaka wapiganaji wa
Al-Shabaab ambao wametajwa kutishia usalama wa nchi.
Matukio ya mashambulio dhidi ya maeneo ya ibada na yenye mikusanyiko ya watu
wengi yamekuwa yakiripotiwa katika siku za karibuni nchini Kenya, na mwishoni
mwa wiki iliyopita watu watatu waliuwawa katika klabu moja mjini Mombasa, baada
ya kushambuliwa kwa magruneti.
0 Comments