Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Servacius Likwelile akichangia mada kuhusu nini kifanyike ili kuimarisha Ofisi ya Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa katika ngazi ya Kitaifa. Katika Mchango wake, Bw. Likwelile amesisitiza kwamba ili Ofisi ya Mratibu Mkazi iweze kutekeleza majukumu yake kikamilifu inatakiwa ijengewe uwezo kwa kuongezewa wataalamu, fedha na vifaa. Amesema kwamba kutokana na Tanzania kuwa moja kati ya nchi Tisa ambazo zimejitolea kushiriki utekelezaji wa Mpango wa Ufanyaji Kazi wa Pamoja wa Umoja wa Mataifa ( Delivering as One) imebaini kwamba kunaumuhimu wa kuiimarisha ofisi hiyo ili kuongeza kasi ya utekelezaji wa majukumu yake na uwajibikaji lakini pia kupunguza urasimu na ukiritimba ambapo kila jambo linatakiwa kutolewa maamuzi kutoka Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa.
Baadhi ya Maafisa kutoka Wizara ya Fedha na Tume ya Mipango wakifuatilia majadiliano yalivyokuwa yakiendelea, majadiliano ambayo pia yalihusisha mjadala kuhusu uboreshaji wa Ofisi ya Mratibu Mkazi ambapo Tanzania kupitia Naibu Katibu Mkuu, Servacius Likwelile licha ya kuelezea umuhimu na faida za Delivering as One hususani kwa nchi zinazoendelea kama Tanzania, alisisitiza kuwa licha ya kwamba kumekuwapo na mafanikio makubwa katika utekelezaji wa mpango huo, lakini imebaini kwamba bado kuna kazi ya kufanya ikiwamo hiyo ya kuimarisha na kuboresha utendaji kazi wa Ofisi ya Mratibu Mkazi wa UM katika ngani ya Kitaifa. Aliyekaa mbele ni Bw. Jerome Buretta kutoka Wizara ya Fedha, Bw. Pastory Masomhe kutoka Tume ya Mipango, Bw. Jimreeves Naftal kutoka Wizara ya Fedha wakiwa na aliyewahi kuwa Mratibu Mkazi wa UN nchini Tanzania, Bw. John Hendra ambaye kwa sasa ni Katibu Mkuu Msaidizi na Naibu Mkurugenzi wa sera na mipango katika Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na Masuala ya Wanawake ( UN-WOMEN).
                                                                   
                                                      Na Mwandishi Maalum

Wakati Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikielezea kuridhishwa na kunufaika na Mpango wa Ufanyaji Kazi wa Pamoja wa Umoja wa Mataifa ( Delivering as One). Imeshauri na kupendekeza kuimarishwa kwa Ofisi ya Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa ili aweze kuwajibika zaidi.

Hayo yamesema na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Bw Servacius Likwelile wakati alipokuwa akichangia majadiliano ya mada kuhusu nini kinahitajika kufanyika ili pamoja na mambo mengine, kuimarisha Ofisi ya Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa ili kurahisisha uratibu na utendaji kazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa.

Bw. Likwelile amewaeleza wachangiaji na washiriki wa Mada hiyo iliyoandaliwa Baraza la Uchumi na Maendeleo ( ECOSOC), katika mkutano unaoendelea hapa UM, kwamba Tanzania ikiwa ni kati ya nchi za mwazo kujitolea kuutekeleza mpango huo kwa majaribio imekwisha kuona manufaa yake kwa kiasi kikubwa.

Akayataja mafanikio hayo kuwa ni pamoja na kupunguza muda na gharama za utendaji kazi na kubwa zaidi serikali kuwa na sauti kubwa katika utoaji wa maamuzi na umiliki wa ajenda zake za maendeleo.

Hata hivyo anasema pamoja na mafanikio hayo na mengine mengi, Tanzania inaamini bado kuna mengi ya kuyafanyia kazi ikiwa ni pamoja na hilo la kuimarisha na kuiongezea uwezo wa kiuwajibikaji Ofisi ya Mratibu Mkazi.

“ Kwa uzoefu tuliopata kupitia mpango huu, niseme kwamba kuna haja ya haraka ya kuchukua hatua madhubuti ya kuimarisha uwajibikaji katika Ofisi ya Mratibu Mkazi. Uimarishwaji huu ni pamoja na raslimali watu, fedha na vifaa na hasa kwa kuzingatia kwamba hapa tunazungumzia Ofisi na si mtu kwa maana ya kiongozi” akasisitiza Naibu Katibu Mkuu.

Akaongeza kwamba hii si mara ya kwanza kutolewa kwa pendekezo la kuimarishwa kwa Ofisi ya Mratibu Mkazi. Kwani hata katika majumuisho ya mkutano uliofanyika huko Montevideo pendekezo kama hilo lilitolewa kinachohitajika ni kulifanyia kazi tu.

Aidha katika mchango wake, Naibu Katibu Mkuu pia amesisitiza haja na umuhimu wa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa kufanya kazi kwa karibu na Ofisi ya Mratibu Mkazi katika ngazi ya nchi ili, si tu kurahisisha utoaji wa maamuzi bali pia kuzifanya ofisi hizo mbili kuzungumza lugha inayofanana. Na hatimaye kupunguza urasimu usiokuwa na sababu.

Aidha wazo hilo la kutaka kuimarishwa kwa ofisi ya Mratibu Mkazi liliungwa mkono pia na wazungumzaji wengine katika mkutano huo. Kwa kusisitiza kwamba Mratibu Mkazi ndiye hasa anayejua nini kinachoendelea au kinashohitajika katika nchi ile anayoifanyika kazi na wala si Afisa aliyeko Makao Makuu.