Wazir Ghazial Sadiq Abdelrahim aliuwawa ajalini
Waziri wa dini wa Sudan Ghazi al-Sadiq Abdel Rahim ni miongoni mwa watu 31 waliouwawa katika ajali ya ndege.
Shirika la habari la Sudan limesema kuwa mawaziri wengine wawili na pia viongozi wa chama kinachotawala cha Omar el-Bashir pia waliuwawa.
Ndege hiyo ya abiria ambayo pia ilikuwa imebeba wakuu kadhaa wa kijeshi ilianguka katika eneo la milima ya Nuba
Ndege hiyo ilikuwa ikielekea eneo la Kordofan ya Kusini kwa sherehe za Eid al-Fitr ili kuuaga mwezi mtukufu wa Ramadhan.
Mbali na waziri huyo wa maswala ya kidini Ghazi al-Sadiq Abdel Rahim wengine waliofariki katika ajali hiyo ni mwenyekiti wa chama, Makki Ali Balayil, waziri wa vijana na michezo, na Issa Daifallah, waziri wa utalii na wanayma pori.

Ndege hiyo ilianguka katika eneo la Talodi huko Kordofan ya Kusini, ikiwa imetoka mji mkuu Khartoum
Mji huo wa Talodi, uko kilomita 50 kutoka mpaka wa Sudan Kusini.
Taarifa za runinga ya taifa zinasema kuwa hali mbaya ya anga iliizuia ndege hiyo kutua na ilipojaribu mara ya pili iligonga mlima.
Afisa mmoja wa shughuli za ndege alisema kuwa ndege hiyo ilikuwa ya aina ya Antonov.
Katika miaka ya hivi karibuni kumekuwa na ajali kadhaa mbaya za ndege.
Maafisa wa Sudan wamekuwa wakilalamika kuwa imekuwa vigumu wao kupata vipuri kwa sababu ya vikwazo vya Marekani.