Serikali ya Ethiopia imesisitiza kuwa nchi hiyo ni tulivu licha ya kifo cha Waziri Mkuu wa nchi hiyo Meles Zenawi aliyekuwa na umri wa miaka 57.
Zenawi alifariki katika hosipitali katika mji mkuu wa Ubelgiji, Brussels, siku ya Jumatatu baada ya kuugua kwa muda mrefu.

Mwili wake unasafirishwa kuelekea mako makuu ya Ethiopia Addis Ababa, na kipindi cha maombolezo ya kitaifa kimetangazwa nchini humo.
Vyombo vya serikali vimeripoti kuwa Makamu Waziri Mkuu Hailemariam Desalegn ndiye atakayeshika madaraka hadi wakati wa uchaguzi mwaka 2015.
Kifo cha Bwana Zenawi kimezua hofu ya kugombania madaraka ambayo ingeweza kuathiri amani ya nchi hiyo.
Ellen Johnson Sirleaf rais wa Liberia amemsifu Bwana Zenawi kuwa alikuwa kiongozi mahiri wa kurekebisha uchumi na pia kiongozi msomi na imara mwenye ushawishi mkubwa barani Afrika.
Naye waziri mkuu wa Kenya Raila Odinga awali aliiambia BBC kuwa ana hofu kuhusu hali nchini Ethiopia kufuatia kifo cha Meles Zenawi kutokana na vita vya kikabila kuendelea kuwa tishio.
Licha ya kuwa kama mmoja wa viongozi wenye ushawishi mkubwa barani Afrika, lakini utawala wake ulikumbwa na utata barani humo.
Hali yake ya afya imekuwa ikiangaziwa kwa majuma kadhaa kabla ya kifo chake ingawaje hakukuwa na thibitisho kuhusu alichokuwa akiugua hasa.
Taarifa ya baraza la mawaziri imesema kuwa Zenawi alikuwa akipokea matibabu ng'ambo na afya yake ilikuwa ikiimarika lakini akazidiwa siku ya Jumapili alipolazimika kurejeshwa hospitalini. Ingawaje madaktari wake walifanya kila wawezalo, alifariki siku ya Jumatatu usiku majira ya saa tano na nusu usiku.
Bwana Zenawi alikuwa kiongozi wa Ethiopia wakati taifa hilo lilipoingia vitani na nchi jirani ya Eritrea mwaka 1998.
Meles Zenawi aliingia mamlakani mwaka 1991 baada ya mapinduzi lakini akapokea sifa kutoka kwa mataifa ya magharibi.