Jenerali Ulimwengu.
HATA kwenye maandiko ya vitabu vitakatifu tunaambiwa kuwa, Mwenyezi Mungu baada ya uumbaji wa dunia alimweka Adamu na Hawa katika Bustani ya Edeni na kuwapa uhuru wa kula matunda yote katika bustani ile isipokuwa matunda ya mti uliokuwepo katikati ya bustani.
Kwa wanaofuatilia maandiko ya dini wanafahamu kilichotokea. Hapa nchini kuna sheria na maneno mengi yanayowataka viongozi na raia wa kawaida kutojihusisha na vitendo vya rushwa.
Lakini ajabu ni kwamba hivi majuzi tumesikia shutuma nzito za vitendo vya rushwa zikitolewa ndani ya Bunge vikiwahusisha viongozi wa Kamati za Bunge hususan Kamati ya Nishati na Madini, Hesabu za Serikali za Mitaa na Hesabu ya Mashirika ya Umma.

Kiukweli tunachokiona si cha ajabu, maana ni taswira ya mambo ambayo sisi kama jamii tumeyakubali, tumeyapokea na kuyafanya kuwa sehemu ya maisha yetu. Limekuwa ni jambo la kawaida mtumishi fulani kula rushwa na kujitajirisha harakaharaka na watu kumsifu kwamba eti ana akili sana!
Katika baadhi ya vitengo kama vile mahakamani, polisi, idara za ardhi au maliasili kama ambavyo iliwahi kuaninishwa na Tume ya Joseph Warioba, ulaji wa mlungula ni tabia ambayo baada ya muda imegeuka na kuwa ‘mazoea’ na hatimaye kuwa haki.
Wanaofanya hivyo wanajiona wana haki ya kupewa rushwa, mahakamani mafaili yanafichwa na hata polisi, sehemu ambazo zilipaswa kuwa mstari wa mbele kutetea haki ya mtu.
Kila mtu pale alipo aiangalie jamii yetu na matendo yake nyakati hizi, naweza kusema kuwa tunaishi katika jamii ya watu wanaopenda rushwa, maana hata bei za bidhaa zipande kiasi gani hakuna mtu anayethubutu kusema kwa sauti kuwa tunalanguliwa!
Kwa kweli inasikitisha zaidi kwa namna Watanzania na serikali yao wanavyoonekana kwa taswira ya rushwa. Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere katika uhai wake na uongozi wake alikemea kwa vitendo rushwa na kwa kiasi kikubwa alifanikiwa kupunguza vitendo vya rushwa nchini.
Kwa msimamo huo huduma za jamii kama vile elimu ilikidhi haja kwani wanafunzi walikuwa wakifundishwa na kugawiwa madaftari na hata kalamu bure, afya- watu walikuwa wakitibiwa bure na dawa zilikuwa zikipatikana, barabara- zilijengwa japokuwa kasi haikuwa kubwa, maji safi na salama yaliwafikia wananchi wengi vijijini bila mizengwe yoyote.
Sifa ya nchi ya Tanzania hakika ilikuwa nzuri machoni mwa wananchi na nje ya nchi. Ilikuwa ni vigumu kuona kiongozi wa serikali au shirika la umma akijenga hekalu ambalo halilingani na mshahara au kipato chake.
Leo hii kiongozi anaweza kusema kwenye bajeti ya serikali kuwa jengo fulani la serikali halitajengwa kwa kuwa bajeti haitoshi lakini huyohuyo akanunua magari yake mawili ya kifahari na kujenga nyumba mbili au tatu. Utajiuliza fedha amepata wapi? Jibu ni rahisi, ni rushwa tu.
Bahati mbaya baada ya uongozi wa Mwalimu, dhambi ya rushwa ikaanza taratibu kutambaa ndani ya jamii na sasa imekuwa kubwa mithili ya kansa isiyotibika. Tunashuhudia rushwa waziwazi katika chaguzi ambapo hata baadhi ya wana habari wanatajwa kujihusisha na rushwa. Hii ni mbaya sana. Wakati mwingine uhitaji hata ushahidi, maana maandishi yao na vitendo vyao vinajionesha.
Nimpongeze mwanahabari mkongwe, Jenerali Twaha Ulimwengu ambaye amewataka wanahabari na wananchi wa Tanzania, hususan wale wanaokerwa na vitendo vya rushwa kukusanya hasira na kukemea kwa nguvu vitendo vya rushwa nchini, namuunga mkono mia kwa mia.
Alisema kuwa, kimsingi huwezi kupigana na mtu au nchi kama huna hasira, vivyohivyo inatupasa kuwa na hasira ya kutosha kupambana na adui huyu aitwaye rushwa ambaye kwa hakika amesababisha mabilioni ya shilingi za walipa kodi kupotea na kuingia katika mifuko ya watu binafsi wasio na huruma na wenzao.
Niseme bila kumung’unya maneno kwamba kama rushwa itaachiwa isambae bila kupigwa vita kwa nguvu, itamaliza taifa, tutateketea.

Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli.