Kocha Mkuu wa Yanga, Tom Saintfiet.
Na Saleh Ally
KOCHA Mkuu wa Yanga, Tom Saintfiet raia wa Ubelgiji, ametangaza kwamba ana hofu wachezaji wake wanaweza kukumbwa na ugonjwa wa shinikizo la moyo ambao unaweza kusababisha waanguke uwanjani na kupoteza maisha. Akizungumza na Championi Ijumaa juzi Oysterbay jijini Dar es Salaam, Saintfiet alisema michuano migumu mfululizo kwa wachezaji wake ni hatari kiafya na inaweza kuwasababishia ugonjwa wa moyo ambao umekuwa ukiua wachezaji ghafla viwanjani duniani kote. “Ndiyo maana nimekuwa nikisisitiza kuhusu michuano ya BancABC Super8, sidhani kama itakuwa vizuri kwa wachezaji wangu kushiriki. Maana itakuwa ni mikubwa na yenye ushindani mkubwa sana. “Wachezaji wa Yanga bado hawajawa fiti, wanahitaji angalau wiki sita hadi saba za maandalizi. Tukilazimisha wanaweza kuingia kwenye matatizo, mchezaji akianguka uwanjani na kufa ni hasara ya Yanga na familia yake. “Tuwalinde wachezaji wetu, najua tunakwenda uwanjani kwa kuwa tutawaona Chuji, Niyonzima, Bahanuzi wakicheza. Sasa kama wataumia kwa kuwa hawapo fiti au kuanguka na kupoteza maisha, siku nyingine mtamuona nani akicheza? Nafikiri naeleweka,” alisema Saintfiet. “Kucheza mashindano si tatizo, lakini kama ingekuwa katika programu, maana yake maandalizi yangefanyika mapema. Angalia Fifa na mashirikisho mengine, leo wanajua mashindano hadi ya miaka mitatu ijayo,” aliongeza Mbelgiji huyo. Akifafanua suala hilo kitaalamu, daktari wa Yanga, Juma Sufiani, alisema ugonjwa wa moyo unaofanya wachezaji kuanguka uwanjani husababishwa na mambo mengi. “Kati ya hayo ni matatizo ya ‘valvu’, matatizo ya mishipa ya damu na maradhi ya misuli ya moyo. Lakini mchezaji kutokuwa fiti kweli ni tatizo mojawapo, maana moyo unafanya kazi saa 24, unapokuwa umelala au upo macho. “Sasa kama haupo fiti, maana yake utataka kujilazimisha kufanya kitu zaidi ya uwezo wako. Hapo unasababisha Hypertension (msukumo wa damu wa juu). Mfano mzuri mimi leo nifanye mazoezi na wachezaji wa Yanga, lazima moyo wangu utazidiwa. Maana yake hata moyo unataka maandalizi, la sivyo ni hatari,” alisema Sufiani na kusisitiza: “Maandalizi ni mazuri, yanajenga uhakika wa kitu, ingawa haiwezi kuwa asilimia 100, kuna wachezaji hupimwa vizuri kabisa kama Fabrice Muamba lakini bado tatizo likatokea, kwa kuwa huo ni ugonjwa, unatokea wakati wowote.” Yanga, Simba na Azam FC zimekuwa zikisuasua kushiriki michuano hiyo kwa madai kuwa zinahitaji kujiandaa kwa ajili ya Ligi Kuu Bara iliyopangwa kuanza Septemba Mosi. |
0 Comments