WADADA wawili mashuhuri katika mchezo wa tennis Venus na Serena Williams wametetea mataji yao mawili waliyoshinda katika michezo ya Olympiki ya Beijing miaka miine iliyopita kwa ushindi wa seti 6-4 6-4 dhidi ya Andrea Hlavackova na Lucie Hradecka wa Jamhuri ya Chek katika mshindano ya Olympic yanayoendelea jijini London Uingereza.

Ushindi huu unamaanisha kuwa Wamarekani hawa wanakuwa ndio wachezaji wa kwanza katika mchezo wa tennis katika historia ya michezo ya Olympic kuwahi kushinda medali katika mashindano matatu tofauti.

Walifanikiwa kushinda medali katika michezo hiyo ilipofanyika katika miji ya Sydney Australia, Beijing Uchina, na sasa London nchini Uingereza.

Tiki Gelana kutoka Ethiopia ameibuka mshindi wa kwanza katika mbio za marathon kilometa 42 wanawake kwa rekodi ya saa 2 dakika 23 sekunde 7 na kupata medali ya dhahabu.

Priscah Jeptoo kutoka Kenya amechukua nafasi ya pili katika mbio hizo akitumia saa 2 dakika 23 nukta 12 na kujinyakulia medali ya fedha.

Naye Tatyana Petrova wa Urusi alishika nafasi ya tatu baada ya kutumia saa 2 dakika 23 nukta 29 na kupata medali ya shaba.

Nao Mary Jepkosgei, Edna Kiplagat Ngeringwony kutoka Kenya na Diane Nukuri wa Burundi hawakufanikiwa katika mashindano hayo.

Jepkosgei alitumia saa 2 dakika 23 sekunde 56, huku Kiplagat akitumia saa 2 dakika 27 sekunde 52. Naye Diane alitumia saa 2 dakika 30 sekunde 13.

Naye Mo Farah wa Uingereza ameshinda medali ya dhahabu mbio za mita 10,000 wanaume katika michezo ya London Olympics 2012.
Farah mwenye umri wa miaka 29 bingwa wa mbio za mita 5,000 alitumia dakika 27 sekunde 30 nukta 42 huku Mmarekani Galen Rupp akishika nafasi ya pili kwa kutumia dakika 27 sekunde 30 nukta 90 na kushinda medali ya fedha.
Tariku Bekele kutoka Ethiopia alinyakua medali ya shaba baada ya kutumia dakika 27 sekunde 31 nukta 43.
Ushindi wa Farah umeizuia Ethiopia kushinda mara nne mfululizo katika mbio hizo na kuzuia Kenenisa Bekele ushindi wa mara tatu mfululizo.
Miaka minne iliyopita jijini Beijing, Farah alishindwa kufuzu fainali za mbio za mita 5000 na toka wakati huo alikusudia kufanya juhudi zaidi.