STAA wa filamu anayetamba katika anga la muziki wa mwambao, Zuwena Mohammed ‘Shilole’ amechafuliwa vibaya na mtu ambaye anatumia jina lake kupitia mtandao wa Kijamii wa Facebook kwa njia ya kujipatia fedha isivyo halali, Risasi Mchanganyiko limeinyaka.
Akizungumza na gazeti hili hivi karibuni, Shilole alisema kuwa kuna mtu amekuwa akitumia jina lake kwenye mtandao huo na kuwaomba marafiki zake wamtumie fedha kwa kuwa mwanaye ni mgonjwa wakati si kweli.
“Jamani huyu mtu ni Shilole feki, tena ananidhalilisha sana kwa kuonesha kuwa nina matatizo wakati si kweli, kama ningekuwa na matatizo ningetumia magazeti na mitandao ingefuata baadaye,” alisema Shilole.
Staa huyo anayetamba na muziki wa mduara alisema kuwa aligundua hila hiyo baada ya kukutana na mtu barabarani na kumpa pole kwa kuuguza mtoto wake na kama alipata michango aliyoiomba kupitia Facebook.
“Natoa taadhari kwa mashabiki wangu wasikubali kumchangia mtu huyo kwani ni tapeli anayetumia jina langu kujipatia kipato, siku nikiwa na matatizo watayajua kupitia magazeti,” alisema.
0 Comments