Wenyeji mjini Kismayo Somalia, wameambia BBC kuwa wapiganaji wa Al-Shabab wameanza kuondoka
katika ngome yao ya mwisho ya Kismayo.

Kismayo ndio ngome kubwa na ya mwsisho ya kundi hilo linalopigana na jeshi la Somalia ambalo limekuwa likiuzingira mji huo kwa usaidizi wa wanajeshi wa AU.
Wenyeji wa mji huo wanasema kuwa wapiganaji wamekuwa wakiutoroka mji huo kwa mabasi huku wakibeba silaha nzito nzito.

Lakini Al-Shabab wamekana ripoti hizo wakisema kuwa wameweza kuwashinda nguvu wanajeshi wa AU.





'Vita vya Propaganda'

Msemaji wa kundi hilo, Muhammad Usman Arus, ameambia BBC kuwa Al Shabaab wamewaua wanajeshi 100 wa Kenya na wa Somalia na kuwaondoa kutoka Kismayo.

"tunadhibiti Kismayo, hizi ni propaganda tu. Wanajeshi wa Somalia na Kenya tayari wameondoka katika maeneo yao'' alisema msemaji huyo.

Wenyeji wa mji huo walisema kuna utulivu ingawa baadhi walidai kuwa kundi hilo limewaacha nyuma vijana ambao wameamrishwa kumuua yeyote anayepinga kundi hilo.

Wanajeshi wa Muungano wa Afrika wamekuwa wakiukaribia mji huo kwa miezi kadhaa sasa.

Wadadisi wanasema kuwa kwa kundi hilo kupoteza udhibiti wa Kismayo, itakuwa pigo kubwa kwao ingawa kundi hilo limesema litaendelea kupigana licha ya hilo kufanyika.

Mnamo mwezi Julai, ripoti ya Umoja wa mataifa, ilipiga marufuku biashara ya mkaa kutoka Kismayo hadi Merca . Biashara hiyo imesaidia Al-Shabaab kupata mamilioni ya dola licha ya baraza la usalama la umoja huo kupiga marufuku biashara ya mkaa kutoka Somalia.

Ripoti hiyo ilishutumu Saudi Arabia miongoni mwa nchi zingine kwa kutozingatia marufuku hiyo na kuendelea kununua mkaa kutoka Somalia.