Baadhi ya Wananchi wa Jimbo la Kitope wakisubiri zamu yao kuingia ndani ya Ofisi ya Jimbo la Kitope kuelezea kero zao kwa Mbunge wa Jimbo hilo Balozi Seif Ali Iddi.
Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Viongozi wa Halmashauri ya CCM Tawi la Pangeni kwenye ukumbi wa Tawi hilo baada ya kupokea kero na changamoto zinazowakabili Wanachama na Wananchi hao wa Pangeni.
Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Seif Ali Iddi alisema licha ya jitihada zinazoendelea kuchukuliwa na Uongozi wa Jimbo hilo lakini bado ipo kazi kubwa ya kufanywa katika kufikia Maendeleo bora ya Wananchi wake.
Balozi Seif alisema hayo mara baada ya kupokea kero na changamoto zinazowakabili Wanachama na Wananchi wa Kijiji cha Pangeni hapo katika Ukumbi wa Tawi la CCM la Kijiji hicho.
Akizungumza na Uongozi wa Halmashauri ya CCM ya Tawi hilo Balozi Seif akiwa pia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema changa moto zinazowakabili Wananchi hao zinaweza kutanzuka kama suala la ushirikiano kati yao na Viongozi wanaowaongoza litapewa nafasi ya pekee.
Balozi Seif alifahamisha kwamba zipo changamoto nyingi ndani ya Jimbo la Kitope lakini kutokana na hali halisi iliyopo ipo haja ya kuziangalia zile muhimu zaidi ili zipatiwe ufumbuzi kulingana na uwezo wa uwezeshaji uliopo.
Balozi Seif pia alielezea faraja yake kutokana na Wananchi wengi wa Kijiji hicho kujitokeza kwa wingi katika zoezi la Uandikishaji wa Sensa ya Watu na Makazi.
Alisema hatua hiyo imesaidia kuliweka katika Historia Jimbo la Kitope pamoja na yeye kupata hadhi zaidi kutokana na nafasi yake ya Uwenyekiti Mwenza wa Kamati Kuu ya Taifa ya Sensa ya Watu na Makazi Tanzania.
Akizungumzia suala la Katiba Mpya ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Balozi Seif aliwaomba Viongozi hao kuwashajiisha zaidi Wanachama wao pamoja na wananchi katika kushiriki kikamilifu kutoa maoni yao wakati utakapowadia.
Othamn Khamis
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.
0 Comments