Maandamano ya kuipinga Japani yameendelea katika miji kadha ya Uchina katika
mzozo unaozidi kuhusu visiwa vilioko katika bahari ya kusini ya Uchina.
Polisi walitumia gesi kutawanya watu waliokuwa na hasira kwenye mji wa
Shenzhen, kusini mwa Uchina, huku waandamanaji wakichoma bendera za Japani
katika mji wa jirani, Guangzhou.
Japan imetoa wito kwa Uchina kuhakikisha usalama wa raia wa Japani, huku
Uchina imezidi kusisitiza madai yake ya visiwa hivo viitwavyo Senkaku au
Diaoyu.
Kwa miaka mingi hayakutokea maandamano ya ghasia Uchina kama haya, kuipinga
Japani.
Watu waliokuwa na hasira walichoma moto bendera ya Japani, walibeba mabiramu
ya kuitusi Japani na kurusha mawe ubalozini.
Karakana na biashara za Japani piya zililengwa na waporaji na kuchomwa
moto.
Hata hivo maandamano hayo hayakutajwa na vyombo vya habari vya taifa na
juhudi zimefanywa kudhibiti majadiliano kwenye internet.
Sababu ni kuwa maandamano yenyewe ni mazuri kufikisha ujumbe kwa Japani,
lakini yanaweza kugeuka na kuwa dhidi ya serikali piya.
Wakuu wa Uchina wanaamini kuwa Japani imevunja makubaliano ya namna fulani,
kwamba hali ibaki kama ilivokuwa.
Serikali ya Japani inasema inavinunua visiwa hivo kutoka serikali ya mji wa
Tokyo ili kuzuwia serikali ya jiji kufanya miradi na kujenga katika visiwa
hivyo.
Lakini Uchina inaona hatua hiyo ni juhudi za kuthibitisha kuwa visiwa hivyo
ni vya Japani. |
0 Comments