Mbunge wa Jimbo la Mtoni (CUF) Mhe. Faki Haji Makame akizungumza kwa niaba ya
waganga wa vurugu za uchaguzi mdogo wa Bububu, mbele ya Katibu Mkuu wa Chama
hicho Maalim Seif Sharif Hamad (kushoto). Picha na Salmin Said, OMKR
Na
Hassan Hamad OMKR
Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi CUF, Maalim
Seif Sharif Hamad amelaani kitendo cha vyombo vya dola kuwapiga na kuwakamata
wafuasi wa chama hicho na kuwaacha wa vyama vyengine na askari waliojeruhi raia
wasio na hatia, siku ya uchaguzi mdogo wa jimbo la Bububu Septemba 16 mwaka
huu.
Akizungumza na wahanga wa tukio hilo huko Makao
Makuu ya CUF Mtendeni mjini Zanzibar jana, Maalim Seif alikiita kitendo cha
askari hao kuwa ni cha kibaguzi kinachoweza kuathiri hali ya maelewano
inayoendelea kudumu Zanzibar.
Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa
Rais Zanzibar, alisema jukumu la vyombo vya dola ni kusimamia haki kwa raia na
si kuwabagua, kama walivyofanya wakati wa uchaguzi mdogo wa Bububu, ambapo
wafuasi wa CUF peke yao ndio waliopigwa na kukamatwa, wakati viongozi na
wanachama wa vyama vyengine walihusika wazi wazi katika vurugu hizo.
“Bila shaka huu ulikuwa mpango wa kupangwa,
wanachama wa vyama vyengine hawakuchukuliwa hatua yoyote, hata Mbunge
hakuheshimiwa na alipigwa kwa sababu tu anatoka CUF”, alisema Maalim
Seif.
Alieleza kuwa katika mazingira ya amani na
maelewano yaliyopo Zanzibar haikutarajiwa baadhi ya viongozi wa serikali na wa
CCM kusimamia askari wa vyombo vya dola, wakiwemo walioficha nyuso zao kwa kuvaa
ninja kuwapiga na kuwakamata wananchi wasiokuwa na makosa kwa njia ya
kibaguzi.
Katika vurugu hizo wafuasi 22 wa CUF akiwemo
Mbunge wa CUF jimbo la Mtoni, Faki Haji Makame walikamatwa na wengine kujeruhiwa
vibaya, katika harakati za uchaguzi mdogo wa jimbo la Bububu, ambapo mgombea
Uwakilishi wa CCM alitangazwa kuibuka mshindi.
Wakati huo huo, Mbunge wa jimbo la Mtoni Faki
Haji Makame amemshitaki Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai na
askari Polisi wa kituo cha Bububu kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, Said
Mwema. Mbunge huyo analalamikia vitendo vya vya uonevu alivyofanyiwa wakati wa
harakati za uchaguzi mdogo wa Bububu na baadaye kubambikiziwa kesi.
Katika barua yake kwa Mkurugenzi wa Mashitaka
Zanzibar ya Septemba 19, ambayo nakala zake zilitumwa kwa Mkuu wa Polisi na
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Mbunge huyo alisema Vuai alishirikiana na
vijana wa CCM waliokuwa wamewekwa tawi la CCM Bububu na baadhi ya Polisi kumwita
kihadaa kumpiga na baadaye kumfungulia mashitaka.
“Wakati nikienda kuwatembelea jamaa zangu kule
Bububu, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar aliniita, nilipofika akawaleta vijana
wa CCM wakanipiga ngwara na nilipowaita Polisi walikuja kunichukua na
kunifungulia mashitaka ya kupigana hadharani”alilalamika Mbunge Makame.
Hata hivyo alisema anashangazwa na kitendo cha
Polisi kuwaacha vijana hapo pamoja na Vuai walioshiriki kumpiga na sasa hajui
anashitakiwa kupigana na nani. Katika barua hiyo aliyoituma jana, alieleza kuwa
vijana hao baadhi yao walikuwa na vipande kadhaa vya kupigia kura waliachiwa na
Polisi kupotea na wala hawana kesi wakati yeye na wafuasi wengine wa CUF
waliteswa na kufunguliwa kesi.
Mbunge huyo anamtaka Mwendesha Mashtaka Mkuu wa
Zanzibar kuchunguza kwa kina tukio hilo, kufuatia malalamiko ambayo tayari
ameshayawasilisha huku akiendelea na taratibu za kuwasiliana na wanasheria wake
kusimamia kesi hiyo.
Mbunge huyo alieleza kuwa ana wasiwasi askari
Polisi Zanzibar wanashirikiana na viongozi na wafuasi wa CCM kukiuka taratibu za
kazi zao za kusimamia haki kwa raia wote.
Katika hatua nyengine, Katibu Mkuu wa CUF,
Maalim Seif Sharif Hamad leo anatarajiwa kuhutubia mkutano mkubwa wa hadhara wa
CUF huko katika viwanja vya Kwa Geji Bububu, ikiwa ni mkutano wa kwanza tokea
kufanyika uchaguzi huo mdogo.
Maalim Seif alikuwa katika ziara ya kikazi
nchini Marekani na Uingereza, wakati uchaguzi huo ulipofanyika, kufuatia kifo
cha aliyekuwa Mwakilishi wa jimbo hilo, marehemu Salum Amour Mtondoo.
|
0 Comments