Sudan na Sudan Kusini zimeafikia makubaliano kuhusu mgogoro wa mpaka na
uzalishaji wa mafuta.
Baada ya mazungumzo ya siku ya nne, nchi hizo mbili zimeafikiana kuruhusu
usafirishaji wa mafuta kutoka kusini kupitia mabomba ya Kaskazini na kuondoa
wanajeshi mpakani.
Viongozi wa nchi hizo mbili hatimaye walikubaliana baada ya mazungumzo ya
siku nne mjini Addis Ababa Ethiopia.
Lakin maswala kadhaa muhimu yangali kutatuliwa ikiwemo kuafikia makubaliano
kuhusu mipaka inayozozaniwa ikiwa ni mojawpao ya kilichosababisha mgogoro ambao
nusura utumbukize nchi hizo kwenye vita mapema mwaka huu.
Baada ya mapigano kuzuka kuhusu mzozo wa mafuta na mipaka, Umoja wa mataifa
ulitishia kuziwekea pande zote mbili vikwazo ikiwa hazitaafikia makubaliano ya
kina.
Wapatanishi wa Muungano wa Afrika wangali kuthibitisha kuwa makubaliano
yameafikiwa lakini rais wa Sudan Omar al-Bashir na mwenzake wa Kusini Salva
Kiir, wanatarajiwa kutia saini makubaliano hayo hii leo.
Maelezo yametolewa tu kwa mukhtasari lakini wapatanishi wa pande zote mbili,
walisema kuwa wamekubaliana kuhusu eneo la nchi hizo mbili ambalo halina ulinzi
wa kijeshi.
Pia makubaliano ya kiuchumi yaliafikiwa kuruhusu Sudan Kusini kuanza tena
shughuli zake za kuzalisha mafuta.
Lakini mwafaka haukupatikana kuhusu eneo linalozozaniwa la Abyei wala mipaka
mingine mingi ambayo nchi hizo zinazozania.
Kwa hivyo makubalino hayo hayajaweza kutimiza masharti ya Umoja wa Mataifa
kwa nchi hizo kuafikia mkataba unaotatua mzozo huo kwa kina. |
0 Comments