Waathiriwa wa shambulizi la kujitoa mhanga mjini Kabul
Takriban watu 12 wameuawa katika shambulizi la kujitoa mhanga dhidi ya basi iliyokuwa imewabeba wafanyakazi wa kigeni karibu na mji mkuu wa Afghanistan, Kabul

Miongoni mwao ni raia wanane wa Afrika Kusini, waliouawa katika shambulizi hilo lililofanyika katika barabara moja kuu inayoelekea katika uwanja wa kimataifa wa ndege.
Kundi la wapiganaji wa Hezb-e-Islami limedai kufanya mashambulizi hayo ambayo linasema ni ya kulipiza kisasi kwa filamu iliyozua ghasia katika nchi za kiarabu kwa kukejeli dini ya kiisilamu.

Shambulizi linajiri wakati NATO ikisema kuwa itapunguza ushirikiano wake na jeshi la Afghanistan kuanzia sasa.


Afisaa mmoja katika wizara ya mambo ya nje ya Afrika Kusini aliambia shirika la habari la AFP kuwa wanane hao waliofariki walikuwa wanafanyakazi wa shirika la kibinafsi la huduma za ndege.

"tumeweza kuwatambua wale waliouawa , lakini hatuwezi kutangza majina yao, hadi tutakapowajulisha jamaa zao'' alisema Nelson Kgwete,msemaji wa idara ya mambo ya nje ya Afrika Kusini.

''hii ni mara ya kwanza tukio la raia wa Afrika Kusini wameuawa katika shambulizi kama hili.''

Bwana Kgwete alisema kuwa haijulikani ikiwa raia wengi zaidi walikuwa katika eneo la shambulizi. Hakutoa tamko lolote ikiwa kuna mipango ya kuwaondoa raia wake katika eneo hilo hadi hali itakapotulia.

Aliongeza kuwa Afrika Kusini haina uhusiano wowote wa kidiplomasia na Afghanistan hali ambayo imetatiza shughuli ya kupata taarifa kwa haraka.

Kwa mujibu wa afisaa huyo, Afrika Kusini inashirikiana na waakilishi wake kupitia maafisa wa Pakistan kujua kinachoendelea.