Kwa mara ya kwanza serikali ya Kenya imekubali kutoa nyongeza ya asili mia 300
kwa mishahara ya walimu ambao wamekuwa katika mgomo wa kitaifa kwa wiki tatu
sasa.Kutokana na maafikiano hayo kati ya serikali na chama cha walimu nchini KNUT,
sasa walimu wanatarajiwa kurejea kazini Jumatatu.
Hatua hiyo sasa itawapa afueni maelfu ya wanafunzi hususan wa shule za msingi
na upili za umma ambao hawajafunzwa wakati huu walimu walipokuwa mgomoni.
Vyama vya walimu nchini Kenya KNUT na Kuppet vilikuwa vikishinikiza serikali
kuwalipa walimu nyongeza hiyo kwa awamu moja.
Awali serikali ya Kenya ilikuwa imekataa kutekeleza matakwa hayo na kuwataka
walimu kukubali kulipwa kwa awamu tatu, awamu ya kwanza ikitekelezwa Oktoba
mwaka huu.
Mwalimu wa chini aliyekuwa akipata shilingi 13,000 sasa atapata shilingi
39.000.
Serikali ya Kenya imetenga zaidi ya dola 159 milioni kuwalipa zaidi ya walimu
250,000 ambao walikuwa wakigoma kulalamikia mishahara duni na mazingira mabaya
ya kazi. |
0 Comments