Waziri wa ulinzi nchini Rwanda, ametuhumiwa kwa kuamuru uasi
katika Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Taarifa hizi ni kwa mujibu wa ripoti
ya wataalamu wa Umoja wa mataifa.
Ripoti hiyo ya kisiri, iliyofichuliwa na shirika la habari la Reuters,
inasema kuwa Uganda pia inaunga mkono waasi wa M23 ambao wamekuwa wakipigana na
jeshi la DRC tangu mwezi Aprili.
Ripoti hii inakuja baada ya ripoti nyingine ya Umoja wa Mataifa kutolewa
mwezi Juni ambayo ilituhumu Rwanda kwa kuunga mkono waasi hao
Lakini Rwanda na Uganda zimekuwa zikikna madai ya kuunga mkono waasi wa
M23.
Duru zinasema kuwa katika kipindi cha miongo miwili iliyopita, Rwanda imeunga
mkono makundi ya waasi Mashariki mwa Congo, kama njia moja ya kupiga vita waasi
wa kihutu waliokimbilia eneo hilo baada ya mauaji ya kimbari mwaka 1994.
Baadhi wanatuhumu Rwanda kwa kutumia waasi kupigana vita vyake dhidi ya DRC ,
nchi ambayo ina utajiri mkubwa wa madini na eneo zima la Maziwa Makuu.
Taarifa za hivi punde za wataalamu wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa
zinatoa maelezo zaidi kuhusu Rwanda kujihusisha na vita vya DRC.
Wataalamu hao wanasema kuwa waasi wa M23 wanapokea amri za moja kwa moja
kutoka kwa mkuu wa majeshi ya Rwanda, Generali Charles Kayonga, " ambaye naye
anafuata amri za waziri wa ulinzi Generali James Kabarebe.
Wataalamu hao pia wanasema kuwa Rwanda imekuwa ikitoa silaha kwa waasi hao na
kuweka mikakati ya kusajili waasi zaidi ili kuliganya kundi hilo kuwa kubwa.
Maelfu ya watu nchini DRC wamepoteza makao yao kufuatia vita hivyo kati ya
waasi na wanajeshi wa Rwanda.
Ripoti hiyo iliyoonwa na shirika la habari la Reuters inasema kuwa wanajeshi
wa Rwanda na Uganda wamesaidia waasi wa M23 kupanua harakati zao katika eneo la
Mashariki mwa DRC. |
0 Comments