Stori: Mwandishi Wetu KUHUKUMIWA kunyongwa hadi kufa kwa MT 1900 Sajenti Rhoda Robert (42) wa Jeshi la kujenga Taifa (JKT- Mbweni), MT 75854 Koplo Ally Ngumbe (37) wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ-Kunduchi) na MT 85067 Koplo Mohamed Rashid (JKT- Mbweni) baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kumuua Swetu Fundikira mwaka 2010 ni mtihani kwa Rais Jakaya Kikwete.Jumanne wiki hii, mbele ya Jaji Zainab Mruke wa Makahama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, washitakiwa hao walikutwa na hatia ya kumuua Swetu na wao kutakiwa kunyongwa hadi kifo. Ili hukumu hiyo itekelezwe ni lazima rais wa nchi aanguke saini ya kalamu kwenye fomu ya hukumu.
Endapo JK atalazimika kuangusha wino kwenye fomu hiyo, atakuwa ameruhusu kunyongwa kwa watu hao watatu katika kipindi cha miaka saba ya utawala wake.
Tangu JK aikamate dola ya Tanzania mwaka 2005, hajawahi kutia saini kwenye hukumu yoyote ya kifo kama ilivyokuwa kwa Rais Mstaafu Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa. Hadi sasa nchini zaidi ya watu 500 wanasubiri kunyongwa.
Mwaka 1998 aliwapunguzia adhabu maafande wawili waliotiwa hatiani kwa kumuua kwa makusudi aliyekuwa Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa, Luteni Jenerali Imran Kombe.
Waliopunguziwa adhabu hiyo kutoka kunyongwa hadi kifungo cha miaka miwili jela ni Koplo Juma Mswa na Konstebo Mataba Matiku.
Rais Mstaafu Ben Mkapa katika utawala wake alibatilisha hukumu za kunyonga watu 100 na kupewa adhabu nyingine ikiwemo kifungo cha maisha.
Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi ndiye pekee aliyesaini utekelezwaji wa hukumu ya kifo kwa watu 21 ambao walinyongwa mwaka 1994.
Utawala wa Awamu ya Kwanza wa Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere alitia saini ya kuwanyonga watu kumi tu.
Kikatiba rais ana uwezo wa kumsamehe mtu aliyehukumiwa kunyongwa ‘Prerogative Mercy’ na kumpa adhabu nyingine.