Rais wa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo, amesema yuko tayari
kuchunguza malalamishi ya wapiganaji wa waasi ambao wameuteka mji wa Goma,
Mashariki mwa nchi hiyo.
Akiongea baada ya mazungumzo yaliyofanyika nchini Uganda na Kuhudhuriwa na
rais wa Rwanda, Paul Kagame, Rais Joseph Kabila amesema anatathmini uwezekano wa
kuanzisha mazungumzo na waasi hao wa M23.
Mwenyekiti na mwenyeji wa Mazungumzo hayo, rais wa Uganda Yoweri Museveni,
rais Kabila na Kagame kwa kauili moja walitoa wito wa kusitishwa kwa mapigano
hayo na pia kutoa amri kwa waasi hao kuondoka Goma mara moja.
Awali wapiganji hao wa waasi walitishia kuendeleza mapigano hayo hadi mji
mkuu wa nchi hiyo Kinshasa.
Hapo jana, wapiganaji hao wa M23 waliuteka mji wa Sake, ulioko takriban
kilomita 27, kutoka Goma. Ripoti zinasema wapiganaji hao sasa wanajiandaa
kuelekea eneo la Kusini hadi Bukavu, takriban kilomita 230 kutoka Goma.
Kamanda mmoja wa waasi hao, aliliambia umati wa watu waliokusanyika katika
uwanja wa michezo mjini Goma, kuwa safari yao ya kukomba taifa hilo
imeanza. Lakini mwandishi wa BBC mjini Goma, anasema haijabainika wazi ikiwa
wapiganaji hao wa waasi wana uwezo wa kutekeleza vitisho vyao.
Kundi hilo la M23 liliundwa mwezi April mwaka huu baada ya wanajeshi kadhaa
kuasi. Wapiganaji hao wa waasi wanasema hawakupewa nyadhifa za kijeshi
walizohaidiwa baada ya kusainiwa kwa mkataba wa amani mwaka wa 2009.
Vitendo vya wapiganaji hao wa M23, vimezua wasi wasi wa kuzuka upya kwa
mapigano nchini Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ambako takriban watu milioni
tano waliauawa kufuatia mapigano yaliyoanza mwaka wa 1997 na kumalizika mwaka wa
2003. |
0 Comments