Mahakama ya Kimataifa ya jinai ya ICC, iliyoko The Hague, imemuachilia huru aliyekuwa kiongozi wa waasi Congo, Mathieu Ngudjolo Chui.
Ngudjolo Chui alifikishwa mbele ya mahakama hiyo mwaka wa 2003, kwa tuhuma za uhalifu wa kivita ikiwa ni pamoja na mauaji ya watu 200 katika Kijiji cha Boogoro, iliyo na utajiri mkubwa wa madini, mkoani Ituri, nchini Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Mahakama hiyo ilifahamishwa ripoti kuhusu watu waliouawa kwa kuchomwa, watoto wachanga kuuawa kwa kurusha ukutani na kubakwa na kina mama.
Bwana Ngudjolo, alikanusha madai kuwa aliidhinisha mashambulio hayo, akisema kuwa alifahamu kutokea kwa mauaji hayo siku kadhaa baada ya tukio hilo kutokea.

Mwendesha mashtaka akosa kutoa ushahidi wa kutosha

Viongozi wa mashtaka walidai Bwana Ngudjolo aliwasajili watoto jeshini ili kutekeleza mauaji hayo.
Lakini jaji anayesikiliza kesi, Bruno Cottes, alisema kuwa mahakama hiyo imemuachilia huru mshukiwa huyo baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha kuwa alihusika moja kwa moja na mauaji hayo.

Mahakama hiyo sasa imeagiza mshukiwa huyo kuachiliwa mara moja.

Mathieu Ngudjolo Chui na Jermain Ntaganda walifikishwa mbele ya mahakama hiyo ya ICC kwa tuhuma za kuongoza, kuidhinisha mauaji ya halaiki pamoja na mashataka mengine kama vile ya ubakaji, kuwasajili watoto jeshi na uhalifu wa kivita.

Mzozo katika eneo la Ituri ulikuwa sehemu ya vita vilivyokumba Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo kufuatia mauji ya kimbari ya mwaka wa 1994, katika nchi Jirani ya Rwanda na ilihusishwa wanajeshi na wapiganaji kutoka mataifa jirani.