Mapokezi hayo yalifunika na kusababisha shughuli mbalimbali kusimama kwa takriban saa 5, huku barabara nyingi na mitaa ikifungwa.Lema alikuwa akirejea Arusha kutoka jijini Dar es Salaam, baada ya Mahakama ya Rufani Tanzania kumrejeshea ubunge wake, aliovuliwa na Mahakama Kuu Kanda ya Arusha Aprili 5, mwaka huu.
Jaji Gabriel Rwakibarila alimvua Lema ubunge, baada ya kuridhika na ushahidi wa wanachama watatu wa CCM, Mussa Mkanga, Agnes Mollel na Happy Kivuyo na mashahidi wao kuwa mbunge huyo alitoa kauli za kashfa dhidi ya aliyekuwa mgombea wa CCM, Dk Batilda Burian.Mbali na nyimbo za kumsifu Lema, wafuasi hao wa Chadema walikuwa wakikiponda Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Msafara wa mapokezi ya Lema aliyevaa fulana nyeupe iliyokuwa na maandishi kifuani yaliyosomeka; ‘Usiogope, Mungu yupo kazini G. Lema’, ulianzia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), ukiwa na magari na pikipiki zaidi ya 100 za wanachama na wapenzi wa Chadema, waliojitolea kuzijaza mafuta na kupakia abiria bila kulipwa.
Shughuli zote za kijamii, zikiwamo safari za magari na biashara katika barabara zote ulipopitia msafara wa Lema, zilisimama kwa muda kupisha msururu huo wa magari na watu kupita, huku waliolazimika kuegesha magari yao pembeni kupisha msafara wakionyesha alama ya vidole viwili inayotumiwa na Chadema.
Msafara kuelekea KIA ulianzia eneo la Phillips jijini Arusha, ukiongozwa na viongozi wa Chadema wilaya na mkoa wa Arusha.
Waliokosa nafasi katika magari ya wanachama na wafuasi wa chama hicho waliamua kusimamisha magari aina ya Coaster, yanayofanya safari kati ya Arusha-Moshi na kuyakodi kwa kujilipia Sh5,000 kama nauli ya kwenda na kurudi KIA.
Baada ya kufika KIA, msafara kutoka Arusha uliungana na uliotoka mkoani Kilimanjaro na kuanza safari ya kurejea Arusha Saa 4:00 asubuhi, safari iliyochukua zaidi saa tano, ambao uliwasili Uwanja wa Soko la Kilombero jijini Arusha saa 9:30 alasiri.
Kwa kawaida, safari kutoka KIA hadi Arusha mjini huchukua dakika 40 hadi 45, lakini jana, safari hiyo ilichukua muda mrefu kutokana na msururu mrefu wa magari, pikipiki na watu waliokuwa wakijitokeza njiani kuusimamisha wakishinikiza kusalimiana na Lema.
Kutokana na hali hiyo, Lema, alilazimika kusimama katika vituo zaidi ya 20 ili kusalimiana na wananchi, ambao wengi wao walishika matawi ya miti mikononi kuashiria amani.
Vituo ambavyo Lema alilazimika kusimama baada ya wananchi kufunga barabara ni pamoja na Njia Panda ya KIA, King’ori, Kikatiti, Maji ya Chai, USA-River, Tengeru, Chama, Kwa Pole, Shangarai, Kambi ya Chokaa, Kwa Mrefu, Ngulelo, Kimandolu, Phillips, Mount Meru Hotel na Sanawari.
Mbunge huyo aliyepanda gari la wazi ili kukata kiu ya wananchi waliokuwa na hamu ya kumwona tangu KIA hadi Arusha mjini pia alisimama katika maeneo ya Clock Tower, Metro Pole, Friends Conner, Kilombero Sokoni kabla ya kuingia kwenye uwanja wa Kilombero National Housing, alikohutubia mkutano mkubwa wa hadhara.
Mapokezi hayo yalihudhuriwa na viongozi kadhaa wa kitaifa wa Chadema akiwamo Mwenyekiti wa Baraza la Vijana (Bavicha), John Heche na wabunge Israel Natse wa Karatu, Joshua Nassari wa Arumeru Mashariki, Cecilia Paresso na Grace Kiwelu wa Viti Maalumu.
Katika hatua nyingine, Chadema, kimetangaza kudai fidia ya zaidi ya Sh250 milioni kwa wanachama watatu wa CCM, waliofungua kesi dhidi ya Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema.
0 Comments