Mhudumu wa chumba cha kuhifadhia maiti hospitali ya Mkoa Singida, akirekebisha mapambo ya jeneza lililokiwa na mwili wa marehemu Munchari Lyoba, mwanafunzi wa SUA , jeneza lililovunjwa na majambazi na maiti kupekuliwa yakitafuta fedha zaidi baada ya kupora wasindikizaji. Picha na Gasper Andrew

WATU wanaodhaniwa kuwa ni majambazi, wamevamia gari lililokuwa linasafirisha maiti kutoka mjini Morogoro kwenda mkoani Mara kisha kupora takriban Sh19.8 milioni walizokuwa nazo waombolezaji.
Katika tukio hilo la kusikitisha lililotokea juzi mkoani Singida, majambazi hao walivunja vioo vyote vya gari pamoja na jeneza lililokuwa na mwili wa Munchari Lyoba aliyekuwa mwanafunzi wa mwaka wa tatu katika Chuo Kikuu cha Sokoine (SUA) cha Morogoro na kumpekua marehemu.
Akizungumza na waandishi wa habari jana nje ya chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Mkoa wa Singida, mkuu wa msafara uliokuwa ukisafirisha maiti, Makaranga alisema kuwa tukio hilo lilitokea juzi saa 7:30 usiku katika gari aina ya Land Cruiser mali ya SUA.
Akisimulia tukio hilo, Makaranga alisema kuwa lilitokea katika Barabara Kuu ya Dodoma – Mwanza nje kidogo ya Mji wa Singida kwenye kona maarufu kwa jina la Mohammed Trans kuelekea mkoani Mara.
Alisema kuwa gari hilo pamoja na jeneza, lililobeba viongozi wa wanafunzi sita na viongozi wengine wanne lilipofika eneo la tukio, walikuta mawe makubwa yamepangwa barabarani na kuwalazimisha kusimama ndipo wakavamiwa na kundi kubwa la vijana, ambao walibeba bunduki mbili aina ya gobore, marungu, mashoka na mawe.
“Walipofika walipiga kioo cha gari letu kwa mbele na kumparaza kwa panga usoni dereva wetu. Baada ya hapo walivunja vioo vyote na kutuamuru kutoa kila kitu tulichokuwa nacho,” alisema Makaranga.
Makaranga alisema kuwa katika tukio hilo, aliporwa Sh2 milioni alizokabidhiwa azihifadhi kwa ajili ya kugharimia msafara huo, Sh8.8 milioni zilizochangwa na wanafunzi kama rambirambi kwa mwenzao na jumla ya Sh9 milioni ambazo wasindikizaji walikuwa nazo mifukoni mwao.
“Pia tuliporwa simu zetu zote za mikononi, viatu, laptop na mabegi yote ya nguo zetu,” alisema.
Makaranga aliyeeleza kuwa anafanya kazi za kiutawala SUA, aliwataja walioumizwa na majambazi hao kuwa ni pamoja na yeye, dereva wao na kiongozi wa wanafunzi, Idd Idd ambao walitibiwa katika Hospitali ya Mkoa wa Singida na kuruhusiwa.
Mkuu wa Wilaya ya Singida, Mwalimu Queen Mlozi, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa amewasiliana na uongozi wa SUA ili watume gari lingine na kukarabati jeneza lililoharibiwa na majambazi hao.
Mlozi aliongeza kuwa kwa ushirikiano wa Jeshi la Polisi na Kamati ya Ulinzi na Usalama, watahakikisha watu waliofanya unyama huo, wanakamatwa haraka iwezekanavyo ili waweze kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria.
“Nimesikitishwa sana na tukio hili, inaelekea sasa binadamu tunaanza kutoka kwenye utu na kuhamia kwenye vitendo ambavyo binadamu wa Mwenyezi Mungu hawezi kuthubutu kuvifanya. Watu wanafikia hata kufungua jeneza na kuanza kulisachi,” alisema Mlozi akionyesha masikitiko.