Nelson Mandela akiwa na waziri wa mambo ya nje wa Marekani Hillary Clinton
Serikali ya Afrika Kusini, imesema kuwa aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Nelson Mandela, bado anaendelea kuzuiliwa hospitalini licha ya kuonekana kuwa amepata nafuu.


Msemaji wa serikali Mac Maharaj, amesema madaktari wanaomtibu Bwana Mandela mwenye umri wa miaka 94, hawana haraka ya kumruhusu kwenda nyumbani.
Mandela alilazwa hospitalini siku 12 zilizopita na amekuwa akipokea matibabu kufuatia maambukizi ya mapafu na uvimbe au mawe kwenye kibofu.
Madaktari wanasema kuwa wameridhika na jinsi rais huyo wa zamani anavyoendelea kupona kwa haraka licha ya umri wake, lakini wamekariri kuwa wanahitaji kumtunza zaidi.

Aliyekuwa rais wa Afrika Kusini Nelson Mandela

 

Mandela shujaa wa uhuru


Bwana Mandela, aliongoza mikakati dhidi ya utawala wa Kizungu kabla ya kuchaguliwa kuwa rais mweusi wa Afrika Kusini mwaka wa 1994.
Aliambukizwa ugonjwa wa kifua kikuu, wakati alipokuwa akizuiliwa katika gereza la Robben Island, ambako alitumikia miaka 18 kati ya 27 alizokuwa amehukumiwa baada ya kupatikana na hatia ya kujaribu kupindua serikali ya nchi hiyo kwa wakati huo.

Ripoti zinasema mapafu ya rais huyo wa zamani yaliharibika wakati alipokuwa akifanya kazi katika chimbo ndani ya gereza.

Mandela bado amesalia kuwa mmoja wa watu mashuhuri zaidi nchini Afrika Kusini, kisiasa hasa wakati huu ambapo chama tawala cha African National Congress kimemchagua Jacob Zuma kuwa kiongozi wa chama na kumrejesha mfanyabiashara tajiri Cyril Ramaphosa kama naibu wake.

Ramaphosa ambaye alikuwa mmoja wa viongozi wa vyama vya wafanyakazi nchini Afrika Kusini, aliibuka na kuwa mmoja wa watu tajiri zaidi baada ya chama cha ANC kushinda uchaguzi.