Rais mteule wa Korea Kusini , Park Geun-hye, amesema ushindi wake katika uchaguzi mkuu utasaidia uchumi wa taifa hilo kuimarika.
Bi. Park, ambaye ni mwanawe, kiongozi wa kiimla wa zamani wa taifa hilo Parl Chung-hee, alimshinda mpinzani wake wa chama cha Liberal Moon Jae-in na kuwa kiongozi wa kwanza wa taifa hilo mwanamke.
Kura bado zinaendelea kuhesabiwa, lakini Bwana Moon amekiri kushindwa.
Idadi kubwa ya watu walijitokeza kupiga kura katika uchaguzi huo ambao masauala ya kiuchumi na kijamii yaliangaziwa pakubwa.
Bi. Park, mwenye umri wa miaka 60, atamrithi Lee Myung-bak, ambaye anastaafu baada ya kukamilisha miaka mitano kama rais wa nchi hiyo kuambatana na sheria za nchi hiyo.
Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na vyombo vya habari nchini humo, mgombea huyo wa chama tawala alipata alisilimia 50 ya kura zilizopigwa naye Bwana Moon, alipata asilimia 48.8.
Ukuaji wa uchumi wa taifa hilo umeshuka kwa asilimia mbili baada ya kukua kwa asilimia 5.5 kwa miongo kadhaa.
Mwandishi wa BBC mjini Seoul anasema, Bi. Park, anakabiliwa na jukumu kubwa la kuunganisha taifa hilo lililogawanyika kwa misingi ya vyama vya kisiasa.