Kamanda wa Polisi Kanda wa Kanda Maaalum Suleiman Kova .

JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limepiga marufuku disko toto katika kipindi cha sikukuu kutokana na kumbi zilizopo kutokidhi mahitaji ya watoto.

Kauli hiyo imetokana na mazoea ya baadhi ya wamiliki wa kumbi za starehe kupiga disko toto inapofika wakati wa sikukuu na kusababisha madhara kwa watoto wanaoingia katika kumbi hizo ikiwemo kufariki kwa kukosa hewa. Akizungumza jijini jana Kamanda wa Polisi Kanda wa Kanda Maaalum Suleiman Kova alisema kumbi zilizopo hazina uwezo wa kukusanya watoto pamoja na kusherehekea kutokana na kumbi nyingi zilizopo hazina nafasi ya kutosha.
“Tunajua fika kipindi hiki wanajiandaa kuweka matangazo ya kuwashawishi watoto waingie katika kumbi zao,ndio nasema ni marufuku kwa mtu yeyote kupigisha disko toto katika kipindi hiki,”alisema Kova.
Alisema lengo la kupiga marufuku disko toto ni kutokana na matukio yanayojitokeza katika kipindi cha sikukuu katika mikoa mbalimbali nchini.
Aidha Kova alizitaka grosari zote zisizo na leseni kusitisha shughuli za biashara kutokana na baadhi ya vibaka kufanya sehemu hizo kama maeneo ya kusubiria kufanya uhalifu.
“Hizi baa za vichochoroni ambazo hazina leseni ndizo wanazopenda kukaa vibaka kwa kuwa wanakuwa hawaonekani na polisi ambao mara nyingi wanakuwapo katika maeneo yaliyo wazi,” alisema Kova.
Pia Kova alitoa wito kwa wananchi kuwa na utulivu katika kipindi cha sikukuu na kuahidi kuimarisha ulinzi kwa kufanya doria katika maeneo yote ya katika ya jiji.
“Tutazidi kuimarisha ulinzi kwa vyombo vya kisasa na kufanya doria za magari,pikipiki,farasi na mbwa waliopewa mafunzo maalum ya kupambana na uhalifu,”alisema Kova.