WATU sita wanaosadikiwa wa familia moja wamefariki dunia mkoani Iringa, baada ya gari walilokuwa wakisafiria aina ya Noah kugonga gari la mizigo na kupinduka. Tukio hilo lilitokea jana saa 6:30 mchana eneo la kizuizi cha matengenezo ya barabara cha Tanangozi, mkoani hapa.
Mashuhuda wa tukio hilo walidai kuwa, gari hilo lilikuwa likitoka Dar es Salaam kwenda Mbeya na kwamba, lilipata ajali wakati lilipojaribu kulipita gari la mizigo lililokuwa mbele yake.
Watu waliofariki ni dereva wa gari hilo, Ezekiel Mwaitebele na mke wake, Grace na Elvis Mwaitebele anayedaiwa kuwa ni mtoto mwenye umri wa miaka miwili.
Wengine ni Linda Ezekiel na Happens anayedaiwa kuwa ni mfanyakazi wa ndani na mwingine ambaye hajatambulika. Kaimu Mganga Mkuu Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa, Dk Faustine Gwanchele alikiri kupokea maiti za watu wanne na kwamba, wawili kati yao walifariki dunia hosptalini hapo.
“Ni kweli tulipokea maiti za watu wanne na wawili walikuwa wamezidiwa sana,mmoja alifariki akiwa mapokezi wakati tukijitayarisha kumhudumia na wa pili alifariki baada ya kufikishwa wodini,” alisema Dk Gwanchele.
Dk Gwanchele alisema maiti zote zimehifadhiwa chumba cha maiti hosptalini hapo, kusubiri taratibu za kupata ndugu zao. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo.
“Imetokea leo (jana) saa 6:30 adhuhuri eneo la Kizuizi cha matengenezo ya barabara eneo la Tanangozi, gari aina ya Noah lililokuwa likiendeshwa na Ezekiel Mwaitebelea liligonga gari la mzigo kwa nyuma na kuanguka na kusababisha vifo vya watu sita papohapo,” alisema Kamuhanda.
|
0 Comments