Jumla ya nchi kumi katika eneo la Maziwa makuu zimekubaliana
kuunda jeshi la pamoja litakalokuwa na jumla ya askari 4,000 katika kukabiliana
na ghasia na vita vya mara kwa mara mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya
Congo.
Waziri wa Ulinzi wa DR Congo, Dakta Crispus Kiyonga amethibitisha uundwaji wa
jeshi hilo, akisema litafanya kazi chini ya usimamizi wa Tanzania.
Mapigano ya hivi sasa mashariki mwa Congo yalizuka mwezi Aprili mwaka huu
wakati waasi wa M23 walipoliasi jeshi la nchi hiyo na kusababisha watu laki tano
kuyakimbia makaazi yao wakihofia usalama wao.
Wakati huohuo, viongozi wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za
Kusini Mwa Afrika, SADC, wameanza mkutano wao wa dharura jijini Dar es salaam
nchini Tanzania.
Wameanza kwa kufanya kikao cha Asasi ya Ulinzi, Siasa na Usalama ya SADC
inayojulikana kama TROIKA chini ya Mwenyekiti wake Rais Jakaya Kikwete wa
Tanzania.
Kwa mujibu wa Waziri wa Mambo ya nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa
Tanzania, Bernard Membe, kikao hicho cha TROIKA kimewakutanisha marais Jakaya
Kikwete, Hifikepunye Phohamba wa Namibia na Jacob Zuma wa Afrika Kusini.
Amesema mara baada ya kikao hicho cha TROIKA viongozi hao watajumuika na Rais
Yoweri Museveni wa Uganda ambaye pia ni mwenyekiti wa mkutano wa kimataifa wa
nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu, pamoja na Rais Armando Guebuza wa Msumbiji
ambaye ni Mwenyekiti wa sasa SADC.
Viongozi hao kwa pamoja watajadiliana kwa kina matatizo ya Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo, Madagascar na Zimbabwe ambapo watawasilisha mapendekezo
yao katika mkutano mkuu wa viongozi wote 14 wa SADC utakaofanyika kesho. |
0 Comments