Mshambuliaji wa Yanga, Didier Kavumbagu (kushoto) akijaribu kumpiga chenga beki wa Black Leopards, Muganga Jean katika mechi ya kirafiki kwenye Uwanja wa Taifa jana. Picha na Michael Matemanga

IKICHEZA soka lenye ‘harufu’ ya Uturuki, Yanga jana iliwathibitishia mashabiki wake ilichojifunza Ulaya baada ya kuiogesha kichapo cha mabao 3-2 Leopards  ya Afrika Kusini katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.
Yanga ilirejea nyumbani mwanzoni mwa wiki hii baada ya wiki mbili za kujifua nchini Uturuki ilikocheza mechi tatu, ikifungwa mbili na sare moja.
Jana Yanga ilikuwa tofauti na ilivyozoeleka awali kufuatia kuonyesha soka lenye ‘taaluma’ na kuwapeleka puta Chui kutoka Bondeni.
Ingawa mchezo huo ulipooza dakika 10 za mwanzo kutokana na kila upande kujaribu kumsoma mwenzake, ulianza kuchangamka ndani ya robo ya kipindi cha kwanza.
Dakika ya 10, nusura Didier Kavumbagu atikise nyavu za Chui hao wa Bondeni kama siyo shuti lake kali kutikisa mwamba wa goli, huku pia akishindwa kufunga dakika ya 22 kufuatia shuti lake kuchezwa na kipa.
Mbuyu Twite angeweza kufunga kwa upande wa Yanga katika dakika ya 25, lakini shuti lake la karibu na lango lilichezwa na kipa wa Leopards.
Shambulizi lingine kali kwenye lango la Leopard lilifanywa dakika ya 52 baada ya wachezaji wa Yanga kushirikiana vizuri lakini wakaishia ‘kumpasia’ mpira mkononi kipa. Leopards wangeweza kusawazisha bao hilo baada ya shuti la Rodney kugonga mwamba wa Yanga dakika ya 24, na akashindwa kufunga tena dakika ya 33 baada ya Ally Mustapha kudaka shuti lake.
Leopards walirejea na kasi kipindi cha pili na kufunga bao la kusawazisha kupitia kwa Humphery Khoza akiunganisha kona ya Abbas Amidu, na kisha kufunga bao la pili dakika ya 88 kwa mkwaju wa penalti kupitia Romagalela baada ya Nadir Haroub kumwangusha ndani ya eneo la hatari Khoza.
Frank Domayo aliifungia Yanga bao la pili dakika ya 63 akimalizia pasi ya Niyonzima, kabla ya Tegete kufunga bao la tatu kwa shuti kali akiwa nje ya 18.
Tegete aliyeng’ara safari ya Uturuki, aliipeleka Yanga mapumziko ikiwa mbele baada ya kufunga bao la kwanza kwa mkwaju wa penalti katika dakika ya 33.
Kiki hiyo ya penalti ilitolewa na mwamuzi baada ya beki wa Leopards, Nkoyiyabu Xakane kumfanyia madhambi  Niyonzima ndani ya eneo la hatari. Kocha Ernets Brandts aliwapumzisha, mapacha Twite na kipa Mustapha na Tegete na kuingia Msuva, Juma Abdul, George Banda na kipa, Said Mohamed.
Wakati huohuo, Mkutano wa wanachama wa klabu ya Yanga, ufanyika leo kwenye Bwalo la Maofisa wa Polisi, Oysterbay Dar es Salaam huku ajenda kuu ikiwa kuzungumzia mapato na matumizi ya klabu.
Yanga ilikuwa katika mgogoro wa uongozi kabla ya kufanya uchaguzi wake Julai 15 mwaka jana.
Ofisa Habari wa Yanga, Baraka Kizuguto alisema jana kuwa, mkutano huo utaanza saa 3:00 asubuhi na kusisitiza wanachama wanapaswa kuwahi ili kwenda na muda.
Kizuguto alisema miongoni mwa mambo watakayozungumzia pia ni ushiriki wa  timu yao wakati mzunguko wa pili wa ligi kuu ukikaribia. Ligi Kuu inatarajia kuanza Januari 26.
Pia ajenda ya mengineyo itakuwa kufahamu idadi ya wanachama hai waliolipia kadi zao kwa wakati.