Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete
amemtumia Salamu za Rambirambi Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo,
Mheshimiwa Dkt. Fenella Mukangara kufuatia kifo cha msanii maarufu wa
kujitegemea hapa nchini, Juma Kilowoko maarufu kwa jina la kisanii la Sajuki,
kilichotokea usiku wa kuamkia tarehe 2 Januari, 2013 katika Hospitali ya Taifa
ya Muhimbili alikokuwa amelazwa kwa matibabu.
Enzi za uhai wake, Marehemu
Juma Kilowoko alianza kujishughulisha na Tasnia ya Sanaa kwa kujiunga na kundi
maarufu la sanaa la Kaole kabla ya kufanya uamuzi wa kuwa msanii wa kujitegemea
ambapo aliendelea kupata umaarufu katika tasnia ya michezo ya kuigiza na filamu
na kufanikiwa kutengeneza filamu nyingi.
Baada ya kuanza kuugua mwaka
2010, Marehemu Kilowoko aliwahi kupatiwa matibabu nchini India mwaka 2011 na
kurejea akiwa amepata nafuu kubwa kiasi cha kumwezesha kutengeneza filamu
nyingine, lakini alianza kuugua tena hadi mauti
yalipomkuta.
“Nimesikitishwa na kuhuzunishwa mno na kifo cha Msanii Juma
Kilowoko ambaye ametoa mchango mkubwa katika kuinua kiwango cha sanaa hususan
michezo ya kuigiza na filamu hapa nchini. Kwa hakika kifo cha msanii huyu ni
pigo kubwa kwa Tasnia ya Michezo ya Kuigiza na Filamu ambayo inaendelea
kujizolea umaarufu mkubwa miongoni mwa Watanzania”, amesema Rais Kikwete katika
Salamu zake za Rambirambi.
“Kutokana na msiba huu mkubwa, nakuomba wewe
Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Mheshimiwa Dkt. Fenella
Mukangara unifikishie salamu zangu za rambirambi na pole nyingi kwa Familia ya
Marehemu Juma Kilowoko kwa kuondokewa na Kiongozi na Baba wa
Familia.
“Natambua uchungu ilio nao Familia ya Marehemu Kilowoko, lakini
nawahakikishia kwamba binafsi niko pamoja nao katika kuomboleza kifo cha mpendwa
wao. Nawaomba wawe na moyo wa uvumilivu, ujasiri na subira katika kipindi hiki
kigumu cha maombolezo. Namuomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema aipokee na
kuilaza mahala pema peponi roho ya marehemu Juma Kilowoko, Amina”.
Aidha
Rais Kikwete ametoa pole kwa wasanii wote nchini hususan wanaojishughulisha na
masuala ya michezo ya kuigiza na filamu kwa kumpoteza mwenzao na hivyo kuleta
simanzi na huzuni kubwa miongoni mwao. Hata hivyo amewataka kuwa wavumilivu na
kuchukulia kifo hiki kama changamoto kwao katika kuendeleza tasnia ya michezo ya
kuigiza na filamu hapa nchini. |
0 Comments