Stori:Haruni Sanchawa TUKISEMA staa wa filamu za
Bongo, Vincent Kigosi ‘Ray’ yamemkuta ni sawa, kisa ni ile ishu yake ya
kutengeneza filamu inayoitwa Sister Marry ambapo mapadri wamemtaka
asiipeleke sokoni milele, Risasi Jumamosi lina mkanda wote. Ishu hiyo
ilitokea kwenye kikao kizito cha saa 5 kilichofanyika Jumanne iliyopita
katika Ofisi za Utamaduni jijini Dar es Salaam. Washiriki wa kikao
hicho walikuwa Ray, Mkurugenzi Mtendaji wa Utamaduni aliyetajwa kwa jina
moja la Mwansoke, mapadri wanne na mtu mmoja aliyedaiwa kuwa ni wa
kutoka Ofisi za Usalama wa Taifa.
Kikao hicho kilikuja baada ya hivi karibuni viongozi wa Kanisa Katoliki
Jimbo Kuu la Dar es Salaam kumtaka msanii huyo ajieleze kimaandishi ni
kwa nini mtawa Sister Marry (Irene Uwoya pichani) alikuwa akifanya
matendo ambayo kiuhalisia, Wakatoliki wenyewe huwa hawayafanyi. Kabla
Ray hajajieleza kwa maandishi ndipo alipoitwa huko na kukubaliana ana
kwa ana na jopo hilo huku mashinikizo kadhaa yakielekezwa kwake. Awali,
wajumbe wote wakiwa wamekaa kwenye viti, filamu hiyo yenye saa 3
iliwekwa mwanzo mwisho huku mapadri hao wakiguna kila wakati, hasa
wakati Sister Marry akiwa anafanya mambo yake mabaya. Baada ya
kumalizika kwa filamu hiyo, hoja zikaanza. Mwansoke akasema vipande
vyote vichafu vinyofolewe na kubaki vile ambavyo wajumbe hawakuvigunia. Baada
ya bosi huyo kusema hayo, mapadri wakasema ‘noooo’. Filamu hiyo isiende
mitaani hata kidogo kwani imejaa udhalilishaji wa Wakatoliki. Inasemekana
Paroko wa Kanisa la Mtakatifu Maximilian Kolbe lililopo Mwenge Kijijini
(jina halikupatikana mara moja) yeye alipigilia msumari wa mwisho kwa
maneno aliyoyatoa. Alisema kwa kuwa filamu hiyo ilirekodiwa kwenye
kanisa lake hilo, anataka vipande vyote vya kanisa hilo vitolewe ndipo
iingie mtaani, jambo ambalo lilimtoa machozi Ray. Ray sasa! Siku ya
Alhamisi iliyopita, Ray alizungumza na gazeti hili na kukiri kuwepo kwa
kikao hicho. Akasema itakuwa vigumu kuviondoa vipande vya kanisa hilo
kwa sababu asilimia 85 ya filamu nzima imerekodiwa Maximilian Kolbe. “Asilimia
85 ya filamu imerekodiwa Maximilian Kolbe, sasa wanaposema niviondoe ni
kuimaliza filamu yote. Filamu ni ya saa 3, ukivitoa vipande vya kanisa
si itabaki dakika 5 tu,” alisema Ray. Alisema kikao kiliisha kwa
maamuzi hayo, kwamba mtu wa utamaduni alisema vipande vichafu
vinyofolewe huku mapadri wakitaka muvi nzima isiende sokoni na paroko wa
Maximilian Kolbe akitaka kanisa lake lisionekane kwenye filamu hiyo. Risasi: “Je, wewe Ray umeamuaje?” Ray: “Sijaamua chochote kwa kweli. Niponipo tu, nimetumia fedha nyingi sana.” |
0 Comments