Rais wa Ufaransa Francois Hollande, amesema nchi yake
iko tayari kusaidia jeshi la Mali kupambana na waasi wanaodhibiti
Kaskazini mwa nchi.
Amesema kuwa ataweza kujibu haraka ombi kwa
serikali yake la kutoa msaada wa kijeshi kwa nchi hiyo ili kusitisha
harakati za wapiganaji hao.
Lakini alisema kuwa wataweza tu kufanya kazi yao ikiwa Umoja wa
Mataifa utawaidhinisha. Umoja wa Matifa hata hivyo ndio umetoa wito wa
kupelekwa kwa wanajeshi wa kimataifa nchini humo katika mkutano wa
dharura wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa.
Rais Hollande, alisema kuwa harakati za
wapigajani hao wanaohusishwa na kundi la Al Qaeda,sasa zinatishia
utahbiti wa Mali. Hadi sasa Ufaransa imesema iko tayari tu kutoa mafunzo
kwa jeshi la Mali.
Awali baraza la usalama la Umoja wa mataifa
lilitoa wito wa kupelekwa kwa wanajeshi wa kimataifa nchini humo ambako
wapiganaji wa kiisilamu wanadai wameuteka mji muhimu wa Konna.
Wakati huohuo, duru za kidiplomasia zinasema
kuwa rais wa nchi hiyo ametoa wito kwa Ufaransa kusaidia katika
kupambana na wapiganaji hao, hoja iliyojadiliwa katika mkutano wa
dharura wa baraza la usalama la umoja wa mataifa.
Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa,
Susan Rice, alihoji ikiwa rais Dioncounda Traore alikuwa ametoa ombi
maalum na kufafanua aina ya msaada anaotaka.
Mwezi jana Umoja wa Mataifa uliidhinisha mpango wa kutuma wanajeshi
elfu tatu kuweza kutwaa eneo la Kaskazini mwa nchi ambalo linadhibitiwa
na makundi ya kigaidi yaliyo na uhusiano na kundi la Al Qaeda.
Wapiganaji wa kiisilamu wameweka sheria kali za kiisilamu katika eneo hilo.
Kwa sababu ya mipango ya usafiri na vifaa ,
kikosi cha wanajeshi wa Afrika hakitatarajiwa kuanza kazi hadi ifikapo
Septemba au Oktoba. |
0 Comments