Stori: Issa Mnally
MTU mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Julius Makene, hivi karibuni alinusurika kichapo kutoka kwa wananchi wenye hasira, baada ya kunaswa akijifanya afisa wa Mamlaka ya Udhibiti wa Vyakula na Madawa (TFDA),Chanzo cha habari kinaweka ushahidi hadharani.Makene alikamatwa maeneo ya Makumbusho, Kijitonyama jijini Dar akikagua duka la vipodozi akidai kutumwa na mamlaka husika na kudaiwa kujipatia shilingi 20,000.
Kwa mujibu wa chanzo chetu, Makene alifika katika duka hilo na kuwakuta akina dada wawili wakiuza bidhaa na kujitambulisha kama afisa wa TDFA na kufanya ukaguzi ambao uligundua bidhaa zisizofaa kwa matumizi ya binadamu.
Inadaiwa kuwa Makene alizidi kuwatetemesha akina dada hao ambao waliingiwa na woga baada ya kuwataka kuambatana na mmoja wao kwenda polisi kama wasipotoa shilingi 50,000.Hata hivyo, hawakuwa na kiwango hicho cha fedha, wakamuomba apokee shilingi 20,000, akakubali.
Wakati Makene akiondoka, ghafla bosi wao alirejea na kupishana naye mlangoni.
Bosi alipopewa taarifa, alimkimbilia na kumtaka kama kweli ni afisa wa TFDA basi amuoneshe kitambulisho lakini Makene hakuwa nacho.
Katika majibishano hayo yaliyokusanya watu wenye hasira, Makene alisema amepata kibali kutoka kwa Afisa Mtendaji wa Kata ya Kijitonyama, wananchi wakamtaka aongozane nao hadi katika ofisi hizo.
Alipofikishwa kwa Afisa Mtendaji wa Kata ya Kijitonyama, John Njunde (pichani) mtuhumiwa huyo  alijitambulisha kama ni Afisa wa TFDA lakini alipobanwa akasema ni mgambo mwenye namba MG 267 baada ya  maelezo yake kumchanganya afisa mtendaji aliamuru Makene apelekwe katika Kituo cha Polisi cha Kijitonyama ‘Mabatini’.
Jambo la kushangaza baada ya Makene kufikishwa  kituoni hapo, alijitambulisha kwa jina la Iddi Likonge na kusema kuwa yeye siyo afisa wa TFDA lakini anashangaa amefikaje  kituoni hapo.