Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
SERIKALI imewasilisha bungeni mapendekezo ya mabadiliko katika
Sheria ya Ukaguzi wa Hesabu za Umma ya 2008, huku ikiongeza vifungu
ambavyo vinapunguza nguvu ya Bunge katika kushughulikia taarifa ya Ofisi
ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Marekebisho hayo yamo kwenye Muswada wa Sheria
ya Mabadiliko ya Sheria, namba 3 ya mwaka 2012 (The Written Laws -
Miscellaneous Amendments Bill) uliowasilishwa bungeni jana na
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema.
Kwa mujibu wa Ibara ya 143 (4) ya Katiba ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, CAG anawajibika kuwasilisha taarifa
yake kwa Rais ambaye baada ya kuipokea atawaagiza watu wanaohusika wawasilishe taarifa hiyo kwenye kikao cha Bunge kilicho karibu.
Taarifa hiyo inabidi iwasilishwe katika kikao hicho kabla ya kupita siku saba tangu siku ile kilipoanza kikao hicho.
Sheria ilivyo sasa inaelekeza kuwa baada ya
ripoti hiyo kuwa silishwa bungeni itajadiliwa katika kamati tatu
zinazosimamia Hesabu za Serikali kwa ajili ya kuifanyia uchambuzi, kisha
kuwasilisha taarifa zake bungeni katika muda zitakazopangiwa.
Kamati hizo za Bunge ni zile za Hesabu za
Mashirika ya Umma (POAC), Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) na Hesabu
za Serikali Kuu (PAC) ambazo hufanya uchambuzi kisha kusoma taarifa zake
ndani ya Bunge kwa hatua zaidi.
Hata hivyo, marekebisho yaliyowasilishwa
Bungeni jana na Jaji Werema yanapendekeza kubadili utaratibu mzima wa
kushughulikia taarifa hiyo, kwani yanaongeza vipengele,
“vinavyoliwajibisha Bunge kwa Serikali” badala ya kinyume chake.
Serikali imeongeza vipengele vya ziada ambavyo
vinazitaka kamati za Bunge zinapofanya uchambuzi wa ripoti ya CAG,
kupeleka maazimio yake kwa Serikali ili “yatafutiwe majawabu” badala ya
utaratibu wa sasa wa kupeleka hesabu zake bungeni.
Kimsingi Kamati za Bunge hufanya kazi kwa
niaba ya Bunge, hivyo taarifa zake husomwa Bungeni na siyo kwingineko
kama ambavyo marekebisho ya sheria yanataka kuelekeza. Jaji Werema
alisema: “Marekebisho haya yamefanywa ili kumwezesha Waziri wa Fedha
kuwasilisha taarifa ya majibu ya Serikali ya hoja za Mkaguzi na Mdhibiti
Mkuu wa Serikali”.
Ikiwa Bunge litapitisha marekebisho hayo ni
dhahiri kwamba Bunge halitakuwa tena na uwezo wa kuwawajibisha watendaji
wa Serikali ambao watabainika kuhusika na upotevu wa fedha au kufuja
fedha za umma, hivyo kupunguza uzito wa mjadala na uwezo wa wabunge
kuhoji.
Kadhalika taarifa za LAAC, POAC na PAC kuhusu
taarifa ya CAG na mapendekezo ya kamati hizo, yatajadiliwa sambamba na
majibu ya Serikali. Hivyo hakutakuwa na nafasi ya Bunge kutekeleza
wajibu wake wa kuisimamia Serikali kama inavyoainishwa katika Katiba.
Hatua hiyo ni sawa na kulifunga Bunge mikono
kutokutekeleza wajibu wake kuhusu ripoti ya CAG, kwani kwa mujibu wa
sheria halitaweza kujadili chochote hadi Serikali kupitia kwa Mlipaji
Mkuu (Paymaster General) atakapokuwa ametoa majibu ya utetezi kuhusu
kasoro katika ripoti hiyo.
|
0 Comments