MOTO wa kuwashtaki kwa wananchi Spika wa Bunge, Anne Makinda na Naibu wake, Job Ndugai uliowashwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) jijini Dar es Salaam Februari 10 mwaka huu, unatarajiwa kuendelea leo mjini Arusha ambapo chama hicho kitafanya mkutano mkubwa wa hadhara.
Mbali na mkutano huo, chama hicho kimesema Katibu wa Bunge, Thomas Kashilillah hana uwezo wa kutoa tamko kuhusu Bunge bila bunge lenyewe kuridhia, kusisitiza kuwa hata spika wa bunge naye hana uwezo wa kuunda Kamati za Bunge na kwamba wanachokifanya viongozi hao ni kudhoofisha Mamlaka ya mhimili huo wa Serikali.
Februari 8 mwaka huu Chama hicho kilitangaza vita kwa kwa viongozi hao wa bunge kwa madai kuwa wamezitupa hoja zilizowasilishwa bungeni na wabunge John Mnyika wa Chadema na James Mbatia wa NCCR-Mageuzi.
Kutokana na hali hiyo kilitangaza kufanya maandamano nchi nzima ili kuwashitaki Makinda na Ndugai kwa kwa wananchi.
Mkutano huo ulifanyika Februari 10 katika viwanja vya Temeke mwisho jijini Dar es Salaam, huku viongozi wakuu wa chama hicho wakieleza yaliyojiri bungeni sambamba na kutaja namba za simu za Makinda hali iliyofanya baadhi ya wananchi kumtumia ujumbe wa matusi.
Akizungumza na Mwananchi Jumapili Katibu mkuu wa chama hicho, Dk Willbroad Slaa alisema awali walitangaza kuwa mikutano hiyo itafanyika katika kanda 10, wanaanza na Kanda ya Kaskazini.
“Tunaanzia Arusha mjini na mkutano wetu utafanyika kesho, atakuwepo Mwenyekiti wa chama taifa, Freeman Mbowe pamoja na viongozi wengine wa chama” alisema Dk Slaa na kuongeza;
“Kila Kanda itakuwa na ratiba zake, lengo letu ni kufanya mikutano na kuwaeleza wananchi ukweli na tutakwenda hadi vijijini.”
Alisema mikutano hiyo kwa kila kanda inaweza kuchukua hadi mwezi mzima, huku akisisitiza kuwa kauli zinazotolewa na Makinda na Ndugai ni udikteta na kutaka kuiridisha Tanzania miaka 50 iliyopita.
Dk Slaa aliponda kitendo cha Makinda kuvunja baadhi ya Kamati za Bunge pamoja na Kashilillah kusema kwamba ofisi yake itazuia kuonyesha moja kwa moja vipindi vya Bunge,  kabla ya juzi kuifuta kauli hiyo kwa maelezo kuwa sasa Bunge litaanzisha Televisheni yake na vituo vingine vitakuwa vikichukua matangazo ya bunge kupitia Televisheni hiyo.
“Nachokifanya Kashilillah ni kinyume na Katiba Ibara ya 18, Katibu wa Bunge hana uwezo wa kutoa tamko la kuzuia jambo fulani bila Bunge zima kuridhia mabadiliko hayo” alisema Dk Slaa na kuongeza;
“Hata Makinda naye hana mamlaka ya kuunda Kamati za Bunge, kifupi ni kwamba wanachokifanya ni kinyume na kanuni ya bunge ya 151(1) na 152(2).”