Askari wa Ufaransa nchini Mali.
Habari kutoka kaskazini mwa Mali zinasema ndege za
kivita za Ufaransa zimeshambulia ngome za wapiganaji wa Kiislam karibu
na mji wa Kidal, kaskazini mwa Mali.
Majeshi ya Ufaransa na Mali yanajaribu kuutwaa
mji huo, ambao ni ngome ya mwisho ya wapiganaji wa Kiislam, kufuatia
kuanguka kwa miji ya Timbuktu na Gao.Mwandishi wa BBC nchini Mali amesema mashambulio hayo yamelenga maeneo ya milimani kaskazini mwa mji wa Kidal, ambako waasi hao wanadaiwa kujificha. Majeshi ya Ufaransa yamekuwa yakijaribu kuutwaa mji huo baada ya kuuteka uwanja wa ndege wa mji huo Jumatano.
Mwandishi wetu amesema waasi wa kikundi cha Tuareg, ambao walikuwa wameudhibiti mji huo, wanaweza kuuachia kwa njia ya mazungumzo.
Askari wa Ufaransa wameudhibiti uwanja wa ndege wa Kidal.
Mashambulio hayo yanafuatia ziara ya Rais Francois Hollande wa Ufaransa nchini Mali Jumamosi.
Rais Hollande amesema majeshi yake yataendelea kuwepo nchini Mali hadi pale majeshi ya Afrika yatakapopelekwa kuilinda nchi hiyo.
0 Comments