Mkuu wa Majeshi ya Polisi Tanzania,IGP Said Mwema.  

MTOTO wa mwenye  ulemavu  wa ngozi,  Mwigulu Magessa  (7) ameshambuliwa  na vijana  watatu wanaodaiwa kuvaa nguzo vilizoficha nguso zao na kumkata mkono wake wa kushoto.
Akizungumza kwa simu juzi, Diwani wa Kata  ya Milepa, Apolinari Macheta alisema tukio hilo lilitokea saa 11:00 wakati  Magesa anayesoma darasa la kwanza Shule  ya Msingi Msia,  Kata  ya Milepa, Bonde la Ziwa Rukwa, wilayani Sumbawanga  akirejea nyumbani.
Macheta alisema Magesa alikuwa  ameongozana na kundi la  wanafunzi  wenzake.
Alisema mtoto huyo amelazwa Zahanati ya Mtowisa, Bonde  la Ziwa Rukwa,  wilayani Sumbawanga kwa matibabu  na kwamba,  hali  yake  inaelezwa siyo nzuri kwani alifikishwa akiwa  amepoteza fahamu.
Akisimulia kisa  hicho, Macheta alisema Kijiji  cha Msia  kimegawanyika sehemu mbili; Msia Center na Msia mashambani.
Alisema Magesa  akiwa  ameongozana  na   kundi  la wanafunzi  wenzake  wakirejea nyumbani Msia Mashambani, ghafla  vijana watatu  wanaodaiwa kuvaa kininja waliwashtua, huku  mmoja wao anadaiwa  kumkimbiza  albino huyo na wengine kuwafukuza  wanafunzi wengine.
“Licha ya wanafunzi  hao kupiga kelele zao  haziweza kusikika  kijijini, kwani walikuwa mbali na makazi ya watu... yule kijana mmoja aliyekuwa akimfukuza   albino akiwa na  panga aliukata mkono wake na kutokomea nao  kusikojulikana,” alisema.
Alisema watoto  walipofika  kwa wazazi, waliwasimulia na kuanza msako  mkali kumtafuta Magesa baadaye walimkuta akiwa  mashambani  huku mkono  wake mmoja ukiwa  umenyofolewa.
Jitihada  za kumpata  Kaimu Kamanda  wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Peter Ngusa hazikufanikiwa baada ya simu zake za mkononi kuita  bila kupokelewa.  Wimbi la mauaji ya albino yalikuwa yamepungua kufuatia serikali kuamua kupambana nayo.
Hata hivyo, kwa wiki mbili zilizopita mkoani Rukwa yametokea matukio mawili ya kukatwa mikono kwa walemavu wa ngozi, hali inayoashiria mauaji hayo kurejea kwa kasi.
Watu wanaojishughulisha na mauaji hayo wanadaiwa kutumwa na waganga wa kienyeji kwa ajili ya biashara zao au kuwasaidia wachimbaji madini kupata madini mengi, dhana ambayo ni potofu inayotakiwa kupigwa vita na kila mwananchi.