Picha ikionyesha tukio lililofanywa na Mbunge wa Tabora Mjini,Aden Rage. |
KAMANDA wa Polisi Mkoa wa Dodoma, David Misime amesema kuwa
wanaandaa jalada la kuhusika kwa Mbunge wa Tabora Mjini, Ismail Aden
Rage kwa ajili ya kuliwasilisha kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).
Kamanda Misime alisema jana kuwa wako mbioni kukamilisha jalada hilo ili walipeleka kwa DPP kwa ajili ya kufikishwa mahakamani.“Ni kweli tumepokea malalamiko ya Chadema na tunaandaa malalamiko ili kuwasilisha kwa mwanasheria na Serikali,” alisema Misime.
Hayo yamekuja kutokana na vurugu zilizotokea kati ya wafuasi wa Chadema na baadhi ya wabunge wa CCM, akiwamo Rage wakati walipokuwa wakigombea mlingoti wa bendera kitendo kilichosababisha watu watatu kujeruhiwa katika tukio hilo wikiendi iliyopita mjini Dodoma.
Hata hivyo, Rage amekana kuhusika na vurugu hizo akisema anaamini uchunguzi kuhusu tukio hilo utamuweka huru kabla au baada ya kufikishwa mahakamani kwa sababu hakushiriki wala kumpiga mwanaChadema aliyetangaza kumshtaki.
“Sikumpiga. Historia yangu inaonyesha kuwa sijawahi kushiriki vitendo vya vurugu wala mapigano kwa sababu yoyote ile. Mimi siyo mhuni wa kupiga mtu. Nilichofanya ni kumlinda yule kijana asipigwe na wanaCCM waliojaa hasira kwa yeye kuingilia mkutano wetu,” alisema Rage, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Klabu ya Simba.
Alisema kada wa Chadema ndiye chanzo cha vurugu hizo zilizoishia kwa kujeruhiwa na wanaCCM baada ya kuvamia eneo la mkutano wa chama hicho.
“Baada ya kuona kitendo hicho, mimi pamoja na Mwenyekiti wa CCM wa Iringa, Deo Sanga, kama viongozi tulimfuata kijana yule na kumsihi asifanye hivyo baada ya kuona vijana wa CCM waliokuwapo eneo lile wanaanza kupandisha jazba ambazo tusingemudu kuzizuia, lakini hakutusikilizwa,” alisema.
Rage alisema baada ya kuona kijana huyo anaanza kushambuliwa na wanaCCM ndipo alipolazimika kuingilia kati kuwaamulia na kumkinga asipigwe na mawe na majabali yaliyokuwa yameshikwa na wanaCCM, ambapo kijana huyo alifanikiwa kuchomoka na kukimbia.
Alisema kabla ya vurugu, kundi dogo la wafuasi wa Chadema lilikuwapo eneo la mkutano wakiwa na bendera ya chama hicho bila kufanya vurugu yoyote, ambapo yeye aliwasihi kuwaacha wasikilize sera za chama hicho kwani mkutano ulikuwa wazi kwa wananchi wote bila kujali itikadi za vyama.
Hata hivyo, picha zilizopigwa na kuchapishwa kwenye vyombo vya habari zilimwonyesha Rage na wafuasi wa CCM wengine wakiwa katikati ya vurugu hizo na juzi uongozi wa Chadema Wilaya ya Dodoma ulitangaza kumburuta mahakamani mbunge huyo kwa tuhuma za kujeruhi, kung’oa na kuharibu mali za chama hicho kikuu cha upinzani nchini.
Kauli ya Rage imetokana na kitendo cha uongozi wa Chadema wa Wilaya ya Dodoma kutangaza nia ya kumshtaki baada ya kumpiga kada wao.
Makada wa CCM na Chadema walipigana Jumapili iliyopita wakati wa maadhimisho ya miaka 36 ya CCM mjini Dodoma.
Vurugu hizo zilizuka baada ya wafuasi wa Chadema kukasirishwa na kitendo cha vijana wa CCM kung’oa bendera yao wakati wakiendesha mkutano kwenye eneo la Mwanga Baa mjini Dodoma.
Wafuasi hao wa Chadema walilazimisha kurudisha bendera yao wakati mkutano ukiendelea, ndipo makada wa CCM waliojumuisha wabunge wa Jamhuri ya Muungano walipoamua kuwapiga kwa kuwarushia mawe wafuasi hao na kusababisha kuumia kichwani kwa kada wa Chadema.
Wabunge wa CCM waliokuwa katika tukio hilo ukiacha Rage ni pamoja na Seleman Jafo, Said Mtanda, Mary Chatanda na Nyambari Nyangwine.
Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai akizungumzia suala hilo alimtetea Rage, akisema alikuwa akiamua ugomvi huo na kama isingekuwa yeye mauaji yangetokea.
“Hakuhusika yeye alikuwa akiamua ugomvi na kama asingekuwepo mauaji yangetokea,” alisema Ndugai.
Katibu wa Wabunge wa CCM, Jenista Mhagama alisema kwamba hajapata taarifa za kuwapo kwa tukio hilo.
0 Comments