Rais wa Ufaransa Francois Hollande anatarajiwa kuzuru Mali, ambako makabiliano ya wiki tatu kati ya waasi na wanajeshi yamekuwa yakiendelea.
Wapiganaji hao walipata pigo kubwa kufuatia mashambulizi ya angani dhidi yao yaliyowalazimisha kutoroka.
Bwana Hollande ataenda mjini Bamako kukutana na Rais wa Mpito Dioncounda Traore.
Aidha rais Holland atazuru Timbuktu,moja ya miji iliyokombolewa na wanajeshi wa Ufaransa wakishirikiana na wale wa Mali, Jumamosi wiki iliyopita.
Hatua ya jeshi la Ufaransa kuingilia hali nchini Mali, zimepelekea kukombolewa kwa sehemu kubwa ya Kaskazini mwa Mali iliyokuwa imetekwa na wapiganaji wa kiisilamu.

Wanajeshi wa Ufaransa, kwa sasa wangali wanaendelea na harakati za kuukomboa kabisa mji wa Kidal, ambao ndio mji uliosalia chini ya wapiganaji wa kiisilamu walioanza harakati zao punde baada ya mapinduzi ya kijeshi kutokea nchini humo mwaka jana.
Bwana Hollande ataambatana na mawaziri wake wa mambo ya kigeni Lauren Fabius, ulinzi Jean-Yves Le Drian na ustawi, Pascal Canin.
Awali waziri wa ulinzi, bwana Le Drian alisema kuwa wapiganaji sasa walianza kutawanyika na hivyo kuashiria wakati muhimu katika msaada wa kijeshi wa wanjeshi wa Ufaransa.
Kwa rais ambaye umaaruifui wake ulikunwa umeanza kudidimia, anayekosolewa mara kwa mara kwa kukosa mwelekeo, hatua ya jeshi lake nchini Mali imepongezwa sana kulingana na mwandishi wa BB C mjini Paris Christian Fraser.
Ushawishi wa rais Hollande umeanza kuimarika kulingana na kura za maoni, lakini swali ni je nini kitafanyika baada ya harakati hizi?
Hatua itakayofuata ni Rais kuandaa ukabidhi wa miji iliyokombolewa kwa majeshi ya Afrika na kuhakikisha uthabiti wa miji hiyo, kwa maandalizi ya uchaguzi mkuu.