WANAFUNZI wa Chuo Kikuu cha Kampala nchini Uganda, wameilalamikia Serikali ya Tanzania kwa kulitoza Sh3 milioni basi lao  kwa madai ya kuzidisha uzito lilipopimwa kwenye mizani wakati likitokea nchini mwao kuja Dar es Salaam kushiriki michezo ya Vyuo Vikuu  vya Afrika Mashariki.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake, mwanafunzi aliyejitambulisha kwa majina ya  Shakur Wahad, aliwaambia waandishi wa habari jijini hapa kwamba  basi lao lilikumbwa na tatizo hilo wakati limebeba wanamichezo.
Alisema  wanashangazwa na utaratibu wa upimaji wa magari katika mizani nyingi Tanzania, tofauti na nchi zingine za Afrika Mashariki.
Alisema basi la wanafunzi lilitozwa Sh3 milioni kwa madai ya kuzidisha mizigo, wakati ukweli lilikuwa limebeba wanafunzi pamoja na mizigo yao
vikiwamo vyakula.
“Kama  nchi hii inataka  kufika mahali ikajivunia kimaendeleo inapaswa kulitazama eneo hilo, tumetoka Uganda, tumepita Kenya hatujakutana na kikwazo chochote hadi tulipoingia Namanga kwa upande wa Tanzania ndipo balaa lilipoanza”, alisema Wahad.
 Aliongeza kuwa  wakiwa katika  mizani hiyo ya Namanga, basi lao lilitozwa faini kwa kuzidisha uzito, na baadaye tatizo kama hilo liliwakuta tena  walipofika  mizani iliyopo njia  panda ya Himo mkoani Kilimanjaro na kisha katika mizani ya Mkata iliyopo mkoani Pwani.
Aidha, alisema matatizo waliyokutana nayo, yanatokana na wao kutofahamu juu ya uwapo wa utaratibu wa upimaji katika mizani jambo lililowafanya waamini kuwa safari yao ilikuwa salama pasipo tatizo lolote hususan linalohusiana na masuala ya matumizi sahihi na sheria za barabara.
“Tanzania ina fursa nyingi za kimaendeleo na kwamba ili iweze kujihakikishia inatimiza ndoto zake kuendelea kukua kiuchumi, ni vyema ikatazama maeneo muhimu yanayochangia kukua kwa uchumi huo ikiwamo njia ya usafirishaji hasa  barabara”, alisema Wahad.
Alipoulizwa kuhusiana na suala hilo, Msemaji wa Wizara ya Ujenzi Martin Ntemo, alisema Wizara inalifuatilia suala hilo ili kufahamu undani wa tatizo walilokutana nalo wanafunzi hao katika mizani na kisha atalitolea ufafanuzi baadae.
Kwa upande wake, Katibu wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania(Taboa), Enea Mrutu,alisema Tanzania inapaswa kujifunza kutoka katika nchi zingine kama kweli ina nia ya kuboresha sekta ya usafiri.