WILAYA ya Simanjiro, mkoani Manyara imepatiwa tani 473.8 za mahindi kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu Kitengo cha Maafa ili kipelekwe kwa watu wanaokabiliwa na njaa iliyotokea baada ya kukumbwa na ukame msimu uliopita.
Akizungumza juzi kwenye Mji Mdogo wa Mirerani,Mkuu wa wilaya hiyo, Cosmas Kayombo alisema mahindi hayo yalitolewa kwa maeneo yaliyokumbwa na ukame na yatauzwa Sh50 kwa kilo.
Kayombo alisema wilaya hiyo iliomba kupatiwa tani 3,000 za mahindi kutokana na wakazi wengi kuwa na upungufu wa chakula baada ya kukabiliwa na ukame msimu uliopita wa kilimo.
Alisema kutokana na kuongezewa kiasi kidogo cha mahindi tani 473.8 tofauti na hitaji lao waliloomba,itawabidi chakula hicho kidogo walichopatiwa wakigawe kwa kuwapa kipaumbele wana kijiji ambao hawakupata zile tani 988 za awali.
Mkuu huyo aliagiza ugawaji huo wa chakula hicho ufanyike kwa uadilifu na atawachukulia hatua kali za kisheria watakaohusika kufuja au kutumia chakula hicho tofauti na maelekezo waliyopatiwa.
“Nadhani wote wameelewa maelekezo yangu na sitarajii kutokea ufujaji wowote kwani si busara wazazi kula chakula cha watoto hivyo natarajia zoezi la ugawaji litakwenda kama lilivyopangwa,” alisema Kayombo.
Kwa upande wake,Makamu Mwenyekiti wa Mamlaka ya Mji Mdogo wa Mirerani, Hussein Msokoto alisema wao walipatiwa kiasi cha tani 222.5 ambazo zitagawanywa kwa watu wanaokabiliwa na ukosefu wa chakula.
Naye,Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kairo.,Wilbert Nyari alitoa ombi kwa Serikali kuongeza chakula hicho kwani hakijatosheleza kwa jamii husika,kutokana na kupatiwa kiasi kidogo cha chakula ilihali mahitaji yao ni makubwa.
Alisema msaada wa maindi uliofika ni mdogo ukilinganisha na mahitaji.