Na Lydia
Churi- MAELEZO

Serikali imewasimamisha kazi na itawafungulia mashtaka ya kijeshi Maafisa
watano wa Jeshi la Polisi nchini kutokana na tuhuma mbalimbali za ukiukaji wa
maadili na taratibu za jeshi hilo.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi
Dkt. Emmanuel Nchimbi (pichani kulia) amewataja waliosimamishwa kazi kuwa ni  Elias Mwita aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa
wa Mbeya, Jacob Kiango aliyekuwa Msaidizi wa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Mbeya na
Charles Kinyongo aliyekuwa Mkuu wa kikosi cha kutuliza Ghasia Mkoa wa Mbeya.

Dkt. Nchimbi amesema leo jijini Dar es salaam kuwa  viongozi hao wamesimamishwa kazi tangu jana kutokana na
kukiuka maadili ya jeshi la Polisi nchini ambapo wanatuhumiwa kwa madai kuwa
walipeleka chumvi na sukari kwenye Ofisi ya Mkemia Mkuu badala ya kilo 1.9 ya
madawa ya kulevya aina ya Cocaine yaliyokamatwa na askari mkoani Mbeya mwezi Machi
mwaka jana.

Waziri Nchimbi alisema vitendo
hivyo vinavyofanywa na viongozi wa jeshi la Polisi vinawavunja moyo na kuwapa
hofu askari wa ngazi ya chini ambao hushindwa kufanya kazi zao kwa uadilifu
unaotakiwa.  

Katika hatua nyingine, aliyekuwa
mkuu wa Upelelezi mkoani Kagera Peter Matagi amesimamishwa kazi na atafunguliwa
mashtaka ya kijeshi kutokana na kukiuka taratibu za kazi kwa kuwabambikiza kesi
zisizo na dhamana wananchi 13 wa kata ya Nyakasimbi wilaya ya Karagwe mkoa wa
Kagera Kutokana na vurugu za kugombea ardhi ambazo hazikuwiana na aina ya
mashtaka walioshtakiwa hali inayoonesha dalili ya uwepo wa rushwa


Waziri Nchimbi alisema wananchi
hao walibambikizwa kesi ya ujambazi wa kutumia silaha ambapo walikaa mahabusu
kwa muda wa miezi miwili na baadaye timu ya uchunguzi iliyoongozwa na waziri
mwenyewe kugundua kuwa mashtaka waliyoshtakiwa hayakuwa sahihi hali ambayo
ilisababisha Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali (DPP) aliifuta kesi.


Aidha, Serikali pia imemsimamisha
kazi aliyekuwa Mkuu wa Polisi wilaya ya Serengeti Paul Mng’ong’o kwa kosa la
kuingia katika Hifadhi ya Mbuga za wanyama ya Serengeti na kupanga njama ya
kuchimba madini aina ya dhahabu ndani ya hifadhi hiyo hali iliyosababisha kiongozi
huyo kushtakiwa  kwenye mahakama ya
kiraia huko Serengeti.


Wakati huo huo Kamishna Msaidizi
Mwandamizi wa Polisi aliyekuwa anasimamia ajira katika jeshi hilo nchini Renatus Chalamila amepewa likizo
ya mwezi mmoja baada ya kutajwa mara nyingi kuhusika na kuwatoza fedha vijana
walioomba ajira ya jeshi la polisi ili awapatie kazi hiyo.


Alisema Chalamila amepewa likizo
hiyo na mapendekezo kupelekwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama
mamlaka ya nidhamu  ili Rais afanye
maamuzi juu ya tuhuma zinazomkabili askari huyo.


Kufuatia hali hiyo jeshi la
polisi limelazimika kuwaondoa katika mafunzo askari wanafunzi 95 waliokuwa
wamejiunga na chuo cha polisi baada ya kubainika kuwa walipata fursa hiyo kwa
kutoa fedha.


Waziri Nchimbi alitoa wito kuwa
Serikali itawaunga mkono askari wanaofanya kazi kwa uadilifu ila watakaoenda
kinyume na maadili na taratibu za jeshi la polisi serikali haitasita
kuwachukulia hatua za kisheria ikiwemo kuwafukuza kazi.


Hatua zilizochukuliwa na Serikali
kwa viongozi wa jeshi la polisi ni sehemu ya makubaliano ya Maafisa waandamizi
wa jeshi la Polisi nchini waliokutana hivi karibuni mjini Dodoma kulinda
maadili ya jeshi hilo na kukabiliana na vitendo vyote vinavyolichafua jeshi
hilo kwa jamii ili  kutatua kero za
wananchi na kuzingatia utawala bora.