Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa. |
Baada ya kusema hayo niseme kwamba watu wenye kufikiri wanajua kwamba elimu ndicho kiungo kinachowaunganisha wanajamii waliopo na wanaokuja kwa maana ya mapokeo na hazina ya utambuzi wa jamii endelevu.
Watu wengi wanalalamikia kufeli kwa wanafunzi wa kidato cha nne mwaka jana nchini kwa sababu wanajua jamii isiyokuwa na elimu ni jamii ya wapita njia, kwa maana wako pamoja kwa muda lakini kila mmoja ana safari yake mwenyewe na safari zao hazihusiani sana.
Nikiangalia mataifa makubwa yaliyopata maendeleo ya kiufundi, kiteknolojia na kiviwanda, naona mifumo ya elimu iliyoasisiwa karne kadhaa zilizopita na ambayo imekuwa ikiboreshwa kila mara kukidhi mahitaji mapya katika mazingira mapya. Lakini, hata inapobadilishwa katika kuiboresha, elimu hiyo haiachi misingi ya awali inayoitambulisha kama elimu ya taifa fulani.
Lakini, pamoja na maboresho yote yanayofanywa mara kwa mara, pamoja na kufuata nyendo mpya za sayansi na teknolojia, misingi ya elimu inayojenga utambulisho wa taifa na uzalendo wa raia haibadiliki.
Hakuna shule ya Waingereza inayofundisha hisabati na kemia bila kufundisha habari za Malkia Elizabeth wa kwanza, William Shakespeare na Oliver Cromwell.
Huko Marekani hakuna shule inayofundisha teknolojia ya dijitali bila kufundisha habari za George Washington na Ujerumani hakuna mtoto wa Kijerumani atakayepita shuleni bila kufundishwa kuhusu Martin Luther na kadhalika. Hivyo ndivyo wafanyavyo wenzetu walioendelea ambao wanajali utambulisho wao kama mataifa.
Tumebaki Watanzania na Waafrika na hii ni kutokana na kutawaliwa na mataifa hayo makubwa ambayo hayakutaka tuwe na elimu ya kujitambua.
Baada ya kupata uhuru, wapo waliodhamiria kujenga mataifa kutokana na kile kilichoachwa na mkoloni, Mwalimu Julius Nyerere akiwa mmoja wao. Nyerere alianza kujenga taifa moja baina ya makabila kadhaa kupitia elimu, lakini kwa sababu warithi wake wameitelekeza elimu, taifa limeanza kumomonyoka kama tunavyoshuhudia sasa.Nilishangazwa sana kuona katika nchi hii, kwa mfano, ukienda shule za msingi kila shule ina kitabu chake cha Hisabati, Jiografia na kadhalika.
Ukimhamisha mtoto wako kutoka shule hii hadi nyingine, ukifika kule utatakiwa utafute vitabu vingine kwani utaambiwa kuwa pale wanatumia kitabu cha mtunzi fulani na siyo yule ambaye vitabu vyake vinatumika katika shule aliyotoka mwanao. Mambo ni shaghalabaghala na hakuna anayejali.
Tabia hii ya kila shule kuchagua kitabu cha mtunzi fulani unaweza kutafsiri kuwa kuna wingu la rushwa. Wahusika wa taaluma hii watambue kuwa kinachojenga taifa ni elimu, ni maadili yanayochangiwa na kila mmoja ndani ya jamii ; ni mitazamo inayoshabihiana miongoni mwa wanajamii.
Kama mambo ni hivyo, kuna ajabu gani wanafunzi wakatofautiana sana katika ufaulu? Hakuna muujiza katika hili. Taifa hujengwa na watu walio pamoja na waliodhamiria kujenga taifa, halizuki hivihivi tu.
Tuache fikra za kizamani kuwa ili taifa liwe zuri na kamili basi eneo lake la ardhi la mipaka yake ionekane vizuri. Elimu ni kila kitu.
Yote haya hufundishwa kupitia elimu iliyoasisiwa na kuendelezwa na jamii husika, si na waziri wa elimu bali na jamii yote ya Watanzania walioafikiana juu ya aina ya elimu ya kuwapa watoto wao na aina ya elimu ya kuirithisha toka kizazi hadi kizazi.
Sisi Watanzania tumeshindwa kuliona hili na hakika kila mmoja ajieleze moyoni kuwa kwamba hatujengi taifa moja. Iwapo tumekubali kwamba kila anayeweza ana hiari ya kuwafundisha wanawe kadiri anavyojua, basi tuelewe kwamba tunajenga mataifa mengi ndani ya nchi moja na tutambue kwamba iko siku mataifa haya hayataiva ndani ya chungu kimoja kitu ambacho ni hatari kwa taifa.
Tunaona siku hizi baadhi ya watoto wa wakubwa wakisomeshwa nje ya nchi, wengine wakisomesha watoto wao katika shule za kimataifa, hali ambayo ni hatari sana kama taifa.Kwa vyovyote basi, wanaofeli au waliofeli mwaja juzi na mwaka jana ni watoto wa masikini na tunajidanganya kwamba tunajenga taifa moja. Hapana, huku ni kujidanganya, tunajenga makundi katika nchi moja na kuna uchoyo wa elimu. Wenye uwezo wanapenda watoto wao wasome shule nzuri na zile shule za walalahoi shauri yao! Tabia hii inaua utaifa.
Tunajenga kundi lenye kupata elimu na lisilopata, hawa ni watu wanaona haya yanayofanyika na wanaweka kwenye kumbukumbu zao. Hatujengi bali tunabomoa.
Ndiyo maana hata michango kuendeleza shule inazorota. Nani atachangia wakati wenye uwezo wote watoto wao wanasoma shule za kimataifa?
Kila mmoja atambue kuwa anachokifanya kuhusu elimu ya mtoto wake anakifanya kwa faida ya miaka mingi ijayo katika nchi yetu na si kwa sababu ya sisi tunaoishi leo. Elimu lazima ijengwe na iwe imara kwa faida ya taifa na siyo kwa mtu mmojammoja.
Tuwe na utamaduni kwa kujenga vitu vya kudumu, siyo katika elimu tu bali hata katika miundombinu, ikiwa ni pamoja na makazi yetu, miji ya kudumu na vijiji vya kupendeza, barabara na njia za reli, bandari, mikondo na mifereji ya maji ya kudumu, na kadhalika.
0 Comments