KATIKA kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani, mwigizaji nyota nchini Jenifer Kyaka 'Odama' amewataka wanawake kuamka na kufanya kazi kwa bidii ili kuweza kuondoa utegemezi katika jamii.
Akizungumza na Mwananchi jana Odama ambaye kwa sasa ni msanii wa kwanza wa kike nchini kumiliki kampuni ya utengenezaji filamu ya J-Film 4 Life alisema kujiamini pekee ndiko kunakomfanya mwanamke yoyote kufikia malengo aliyojiwekea katika maisha.
"Kesho (leo) ni siku ya wanawake duniani, lakini tujiulize ni nini tunakifanya katika kuhakikisha tunasonga mbele? Au kila siku tutaogopa kufanya jambo tukitegemea wanaume pekee ndio wenye uwezo?
Tunapaswa kujituma kwa bidii katika kuhakikisha tunatimiza malengo yetu tuliyojiwekea katika maisha,"anasema Odama.
Anasema mwanamke ni kila kitu "kila mtu amezaliwa na mwanamke, huyu ni mtu wa muhimu katika jamii. Bila kujiheshimu na kufanya kazi kwa bidii utu wetu hauwezi kutambuliwa, tunapaswa kuwa na ubunifu."
Ametoa wito kwa kila mwakamke kwa nafasi yake na kwa kazi yake anayoifanya kuongeza bidii zaidi.
Aidha anasema wasanii wengi wa kike wamekuwa wakihofia kujituma na kufanya kazi ambazo wanaume wanazifanya jambo linalochangia kuwarudisha nyuma huku tatizo hilo likisababisha uchache wao katika fani hiyo.