Wakati Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Wilfred Lwakatare anatarajiwa kufikishwa mahakamani leo, jana mchana ofisi za makao makuu ya chama hicho zilipekuliwa na polisi na kuondoka na nyaraka mbalimbali.
Tukio hilo lilitokea jana ikiwa ni mwendelezo wa upelelezi wa tuhuma zinazomkabili Lwakatare ambazo zinazomhusisha na picha ya video iliyorushwa kwenye mitandao ya kijamii. Lwakatare alikamatwa Jumatano iliyopita akihusishwa na picha hiyo iliyomwonyesha Lwakatare akiwaelekeza watu ambao hawakuonekana, kufanya vitendo vya uvunjifu wa amani au uhalifu.
Upekuzi katika ofisi
Polisi hao wakiwa na Lwakatare na mmoja wa mawakili wake, Nyaronyo Kicheere walikwenda kwenye ofisi za Chadema saa 9.00 alasiri kwa ajili ya kufanya upekuzi.
Upekuzi huo uliendeshwa zaidi kwenye ofisi za Lwakatare kwenye Makao Makuu ya Chadema yaliyoko Mtaa wa Ufipa, Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Upelelezi wa kesi hiyo unaongozwa na Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Obadia Jonas. Uchunguzi wa gazeti hili unaonyesha kuwa upekuzi huo ulikuwa na lengo la kupata hati zenye mwandiko wa Lwakatare ili kufananisha na nyaraka mbalimbali walizonazo polisi. Kwa nyakati tofauti, Nyaronyo Kicheere na Ofisa Habari Mwandamizi wa Chadema, Tumaini Makene walithibitisha juu ya upekuzi huo.
Kicheere alisema aliitwa jana kwenda Kituo Kikuu cha Polisi, alipofika alielekezwa kufuatana na mteja wake na polisi kwenda Makao Makuu ya Chadema.
“Walifanya upekuzi kusaka nyaraka kwa ajili ya kuongeza ushahidi wa uchunguzi wao,” alisema Kicheere.
Naye Makene alikiri kufanyika kwa upekuzi na kufafanua ulifanyika ndani ya ofisi za Chadema.
Lwakatare kufikishwa mahakamani
Pia kwa nyakati tofauti Kaimu Mkurugenzi wa Upelelezi, Isaiah Mungulu na Msemaji wa Polisi, Advera Senso waliithibitishia Mwananchi kuwa Lwakatare atapandishwa kizimbani leo.
“Upelelezi umekwenda vizuri na kesho (leo) atapandishwa kizimbani ili kujibu mashtaka yanayomkabili,” alisema Mungulu.