Waziri wa Maendeleo ya Jamii,Jinsia na. Watoto Mhe Sophia Simba ( Mb) akiongoza ujumbe wa Tanzania wakati wa ufunguzi wa  Mkutano wa 57 wa Kamisheni kuhusu Hali ya  Wanawake ( CSW) mkutano huo wa wiki mbili umeanza siku ya jumatatu hapa makao makuu ya Umoja wa Mataifa, wengine katika picha ni Balozi  Tuvako  Manongi, Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Mhe.  Engera Kileo Mmari Jaji wa Mahakama ya Rufa, Naibu Mwakilishi wa Kudumu, Balozi Ramadhan Mwinyi, wengine ambao wapo katika meza  hiyo ya Tanzania, ni  Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Bi. Kijakazi Mtengwa  na Mhe. Imani Aboud Jaji wa Mahakama ya Rufaa. 

Na Mwandishi Maalum

Mkutano  wa  57
wa  Kamisheni ya Umoja wa Mataifa Kuhusu
Hali ya Wanawake (CSW),  umeanza siku ya
jumatatu hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa.


Mkutano huo  wa wiki mbili  na ambao hufanyika kila mwaka unawakutanisha Mawaziri
 wanaohusika na masuala ya wanawake na
maendeleo ya jamii kwa ujumla,  wataalamu
mbalimbali vikiwamo vyama visivyo vya kiserikali kutoka  duniani kote.


Ujumbe wa  Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  katika
mkutano huu unaowajumuisha washiriki kutoka Serikali  ya Mapinduzi Zanzibar  unaongozwa na Waziri wa Maendeleo ya Jamii,
Jinsia na Watoto, Mhe. Sophia Simba ( MB).


Miongoni mwa wajumbe wa
Tanzania  ni  Bi Kijakazi Mtengwa, Katibu Mkuu Wizara ya  Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Bi.
Fatma Gharib Bilal, Katibu  Mkuu, Wizara
ya  Ustawi na  Maendeleo ya Jamii,     Vijana,Wanawake, na  Watoto,
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Majaji wa  Mahakama ya Rufaa, Mhe. Engera Kileo Mmari na
Mhe. Iman Daud Aboud.


Akifungua mkutano huu, Naibu
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bw. Jan
Eliasson amesisitiza kwa kusema, vita
vya kuutokomeza   ukatili dhidi ya
wanaweke lazima iwe ya kufa na kupona.


Akaeleza kwamba  ukatili dhidi ya wanawake ni jambo  linalotokea kila mahali hata katika nchi  zilizoendelea.

Akabainisha kwamba ili
kukakibiliana na ukatili dhidi ya wanawake, panahitajika  mbinu mchanganyiko   kuanzia serikalini kwa kutekeleza sera za
kuwawezesha waathirika wa vitendo hivyo , kuwaadhibu wahalifu


Akaeleza pia kwamba,  wanaume na watoto wa kiume wanatakiwa kuhamasishwa
kushiriki katika kupiga vita ukatili dhidi ya wanawake ikiwa ni pamoja na
kuwajengea utamaduni wa kuwajibika katika shughuli mbalimbali za kifamilia.


Akaeleza  zaidi kwamba,
vitendo hivyo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto  wakike vinafanyika katika  maeneo yenye vita na migogoro lakini pia
vinafanyika katika nchi zenye amani na utulivu. Na kama hiyo haitoshi
vinatendeka pia kwenye miji mikuu   na
halikadhalika vijijini.


“Ni vitendo”
anasema Naibu Katibu Mkuu. “Vinavyotokea katika maeneo ya wazi na yaliyojificha
pia. Na kwa kuwa ni jambo lisilokubalika katika maisha yetu ya kila siku,
tunawajibika kulishughulikia kwa nguvu zote kila mahali na katika ngazi zote”.


Kwa mujibu
wa  Taasisi ya  UN-WOMEN zaidi ya asilimia 70 ya wanawake
katika baadhi ya nchi ni wahanga wa
ukatili au ukatili wa ngono katika maisha yao. Na katika nchi kama vile
Australia, Canada, Israel, Afrika ya Kusini na Marekani asilimia kati ya 40 na
70 vifo vya wanawake vinasababishwa na
masuala  ya mapenzi.


Naye  Mkurugenzi Mtendaji wa  UN-WOMEN Bi. Michelle Bachelet amewaeleza
wajumbe wa  Kamisheni hiyo kwamba, dunia
haiwezi tena kuendelea  kuhimili gharama
za vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto.


Akaongeza
kwamba ni wakati muafaka  na wa haraka
kwa serikali kuchukua hatua dhidi ya vitendo hivi ambayo anasema vinaendelea
kulalamikiwa katika jamii


 Mwenyekiti wa CSW  Balozi Marjon Kamara ambaye ni Balozi  wa Liberia  yeyé amesema katika wiki mbili za mkutano huo
wajumbe watajadiliana na kubadilishana mawazo kuhusu mbinu mbadala na
zinazotekelezeka za kuzuia ukatili dhidi ya wanawake na watoto wa  wakike,
mbinu ambazo kweli zitaweza kuleta matokeo.


Pamoja
na Ujumbe wa Tanzania  kushiriki  kikamilifu katika  mikutano na mijadala mbalimbali ambayo imo
ndani ya  ratiba kuu ya    CSW.
Tanzania  nayo itakuwa na  mijadala yake miwili ( side Events), kwa
lengo la kuonyesha uzoefu wa Tanzania katika kukabiliana na  ukatili dhidi ya wanawake na watoto wa kike


Mjadala
wa kwanza  umeandaliwa na washiriki
kutoka Tanzania Visiwani,    mada yake
itahusu: Vunja ukimya, unga mkono juhudi
za sekta mtambuka katika  kuzuia na
kukabiliana na unyanyasaji dhidi ya wanawake;
uzoefu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; mfano wa Zanzibar.


 Na
mjadala wa pili   umeandaliwa na Chama cha Majaji Tanzania,
utajadili kuhusu: Ukomeshaji wa matumizi
mabaya  ya mamlaka kwa madhumuni ya
kudhalilisha  kingono ( sextortion);
Uzoefu wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania.