Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki moon ameitaka Korea ya kaskazini kupunguza makali yake kwa mzozo unaotokkota wa kinuklia akisema kuwa umeanza kuvuka mpaka.

Bwana Ban amesema kuwa anahuzunishwa na namna ugomvi huo unavyotishia maisha ya wananchi wa kawaida.

Akizungumzia vitisho vya karibuni sana vya Korea Kaskazini kwa Korea Kusini na Marekani, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon alisema kuwa hali hiyo imekuwa ya kustajabisha na kusikitisha.

Alisema kuwa Korea Kaskazini imezidisha vitisho vyake na akaonya kuwa cho chote kinaweza kuzusha kitendo cha kusikitisha.



Bwana Ban aliyekuwa wakati mmoja Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Umoja wa Mataifa, alitoa wito kwa viongozi wa Korea kaskazini kubadili mwenendo wao.
Awali msemaji wa Wizara ya mashauri ya Kigeni wa Urusi alisema kuwa uamuzi wa Korea Kaskazini kuendeleza mpango wake wa kuimarisha uwezo wake wa zana za kinukilia unavuruga mipango ya kuanzisha upya mashauriano yanayohusu mataifa sita ya kupatanisha Korea Kusini na Kaskazini.

Mataifa yanayokusudiwa kushiriki katika mashauriano hayo ni Korea Kusini, Korea Kaskazini, Uchina, Urusi, Japan na Marekani.

Msemaji huyo alieleza kwamba juhudi zo zote za kupuuza maazimio ya Umoja wa Mataifa hazikubaliki.