Dodoma.
 Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe amesema kuwa watakata rufaa katika Kamati ya Kanuni ya Bunge dhidi ya mwongozo wa Spika uliobariki adhabu ya kuwatimua kwa siku tano wabunge sita wa Chadema kwa kudharau mamlaka ya Spika.
Akitoa mwongozo wake jana, Spika Anne Makinda alibariki wabunge hao kutimuliwa akisema kuwa Kanuni za Bunge zilikiukwa.
Wabunge waliofukuzwa na Naibu Spika, Job Ndugai juzi ni pamoja na Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi, Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa, Mbunge wa Ilemela, Highness Kiwia, Mbunge wa Nyamagana, Ezekiah Wenje na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema.
Juzi Mbowe aliomba mwongozo wa Spika kwa kutumia Kanuni ya 68 (7), akimtaka Spika aeleze naibu wake (Ndugai) alitumia kanuni gani ya Bunge, kuwasimamisha siku tano wabunge sita wa Chadema wasihudhurie vikao vya Bunge vinavyoendelea.

Mwongozo wa Makinda
Akitoa mwongozo huo jana, Spika Anne Makinda alisema kuwa kitendo kilichotokea hakiwezi kupuuzwa na wala kuvumiliwa na Bunge, pamoja na wananchi kwa kuwa ni utovu wa nidhamu ya Bunge na wananchi kwa jumla.

Alisema: “Kanuni ya 2(2) na 5(1), inampa mamlaka Spika ya kuleta amani bungeni.
Kanuni ya 2(2) inaeleza: “Iwapo jambo au shughuli yoyote haikuwekewa masharti katika kanuni hizi, Spika ataamua utaratibu wa kufuata katika jambo au shughuli hiyo, kwa kuzingatia Katiba, Sheria nyingine za nchi, kanuni nyingine zilizopo, maamuzi ya awali ya maspika wa Bunge na mila na desturi za uendeshaji bora wa shughuli za Bunge na uamuzi huo utaingizwa katika kitabu cha maamuzi ili kuongoza mwenendo wa baadaye wa uendeshaji wa shughuli za Bunge.”

Kanuni ya 5(1) inaeleza: “Katika kutekeleza majukumu yake yaliyotajwa katika Ibara ya 84 ya Katiba, Spika ataongozwa na kanuni hizi na pale ambapo kanuni hazikutoa mwongozo, basi Spika atafanya kazi kwa kuzingatia Katiba, Sheria nyingine za nchi, kanuni nyingine zilizopo, maamuzi ya awali ya maspika wa Bunge pamoja na mila na desturi za mabunge mengine yenye utaratibu wa kibunge unaofanana na utaratibu wa bunge la Tanzania.”

Makinda alisema kwa kutumia kanuni hizo mbili anakubaliana na uamuzi uliotolewa na Ndugai na kwamba suala hilo litaingizwa kwenye kitabu cha uamuzi wa Spika.

“Natumia Kanuni ya 2(2) na 5(1) kusema kuwa uamuzi uliofanywa na Ndugai ni halali na itaingizwa kwenye kitabu cha maamuzi ya Spika,” alisema Spika Makinda.
Kauli ya Mbowe
Mbowe jana alilieleza gazeti hili kuwa uamuzi wa Spika ulijielekeza katika jambo lisilo na kanuni inayolisimamia, tofauti na lile la kudharau mamlaka ya kiti cha Spika, lililotolewa maelekezo na Kanuni ya 74 (1).

Kanuni hiyo inasema: “Spika anaweza kutaja jina la mbunge kwamba amedharau mamlaka ya Spika na kisha kupeleka jina hilo kwenye Kamati ya Maadili na Madaraka ya Bunge; ikiwa kwa maneno au vitendo mbunge huyo anaonyesha dharau kwa mamlaka ya Spika; au Mbunge huyo atafanya kitendo chochote cha makusudi cha kudharau shughuli ya Bunge au mbunge yeyote anayeongoza shughuli