Katika hali isiyokuwa ya kawaida,  mwanamuziki wa kizazi kipya, Nasibu Abdul’ Diamond’ aling’ang’ania kubaki ndani ya chumba chenye mwili wa marehemu  hata baada ya  tangazo la kuwataka watu watoke.“Nimemshangaa sana Diamond,  wenzake wote tumetoka ndani lakini yeye kang’ang’ania kubaki na maiti,” alisema mwombolezaji mmoja.

WINGI WA AKINA MAMA WASHANGAZA WENGI
Katika msiba wa marehemu Bi. Kidude, umati wa wanawake uliwashangaza wanaume licha ya kwamba ni kawaida kwa wanawake kuwa wengi msibani.
Mwili wa marehemu ulipofika nyumbani kwake, Raha Leo kutoka Bububu ulilazwa katika kitanda cha kamba kama mila na desturi za Pwani zinavyotaka na kisha kupelekwa kuswaliwa katika Msikiti wa Mwenye Shauri kabla ya kupelekwa makaburini.

UPEPO MKALI
Wakati mwili wa marehemu ulipokuwa ukishushwa kuingizwa kaburini, kwa takribani dakika tano ulitokea upepo mkali na kuwafanya baadhi ya watu kushtuka na kujiuliza ni kitu gani.
Wengi walishindwa kupata jibu na kubaki kuamini kwamba upepo huo ulitokana na uzito wa msiba huo mzito.
WALIOHUDHURIA


Ukiachilia mbali watu wa kawaida, watu wengi maarufu wakiongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dokta Jakaya Mrisho Kikwete na Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dokta Ali Mohammed Shein walifika kwenye msiba wa marehemu Bi. Kidude na mazishini pia.
Wengine ni wanamuziki mahiri wa muziki wa Kizazi Kipya Farid Kubanda ‘Fid Q, Diamond, Aisha Ramadhan ‘Mashauzi’, Khadija Kopa na Mkurugenzi wa Vipindi wa Redio na Runinga ya Clouds ya jijini Dar es Salaam, Ruge Mutahaba.
ALIPOPUMZISHWA
Marehemu Bi. Kidude alizikwa majira ya mchana kwenye Makaburi ya Kitumba visiwani humo na hivyo kuhitimisha safari ya uhai wake hapa duniani.
Mwenyezi Mungu aiweke roho yake mahali pema peponi. Amina.