Jengo la Chuo Kikuu Dodoma(Udom) moja ya vyuo vitakavyo tumika katika utaratibu huo mpya 

Dar es Salaam.
 Tume ya Vyuo Vikuu Nchini (TCU), imepanga kuanza kuwadahili wanafunzi wa kujiunga na masomo ya vyuo vikuu kwa kutumia uzoefu wao.
Udahili huo utakaoanza mwaka huu wa masomo 2013/14, utakuwa ukiwahusisha wale ambao elimu yao imeishia darasa la saba na kuendelea, lakini walikosa sifa ya kuendelea na masomo kwa ngazi ya chuo kikuu.
Kupitia utaratibu huo mpya, mtahiniwa atajiunga na Chuo Kikuu kulingana na fani atakayoiomba na atatakiwa kufanya mitihani mitatu na kufaulu kwa wastani wa daraja B.
Mkurugenzi wa Ithibati na Ubora wa Elimu ya Juu kutoka TCU, Dk Savinus Maronga aliliambia gazeti hili kuwa baada ya kuona kuna watu wengi wanaopenda kuendelea na masomo ya elimu ya juu, lakini wameshindwa kutokana na kutokuwa na vigezo, TCU imeamua kuanzisha mitihani hiyo maalumu.
Alisema kuwa mfumo huo unaojulikana kama ‘Recognition of Prior Learning’ (RPL), utamwezesha mwombaji kudahiliwa vyuoni kupitia tume hiyo kama wanavyofanya watahiniwa wengine.

Sifa zinazotakiwa
Kuhusu sifa za kujiunga, Dk Maronga alisema kuwa mwombaji anatakiwa kuwa na umri kuanzia miaka 25 na kuendelea, sambamba na kuwa na elimu isiyopungua darasa la saba.

“Mwombaji anatakiwa kuwa na nia ya kujiunga na elimu ya chuo kikuu na uzoefu wa kile ambacho anakusudia kukisoma.

Awe na uwezo wa kuandika na kusoma Lugha ya Kiingereza, ambayo ndiyo inayotumika kufundishia vyuoni,”alisema Dk Maronga na kuongeza:

“Kuna watu wameishia darasa la saba, lakini wamefanya kazi katika eneo moja, mfano karani wa mahakama, mwandishi wa habari kwa muda mrefu. Hivyo mfumo huu utawawezesha kuendelea na masomo bila tatizo.”

Vigezo
Mkurugenzi huyo alisema, kutakuwa na mitihani ya masomo matatu, ambayo mtahiniwa ili apate nafasi ya kuendelea na masomo ni lazima afaulu kwa wastani wa daraja B.

Alisema daraja la kwanza linaloanza na alama A ni 75-100, daraja B+ ni 60-75, B ni 50-59, C ni 40-49, D ni 35-39 na daraja E ni 0-34.

“Katika mitihani mitatu atakayoifanya, atatakiwa kupata wastani wa daraja ‘B’ na somo husika la fani yake atatakiwa kupata alama B ili kuwa na vigezo vya kupata cheti kitakachomwezesha kuendelea na masomo yake,”alisema Dk Maronga.