Zanzibar.
 Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad amesema Serikali italazimika kuchukua hatua za dharura katika kukabiliana na wafanyabiashara wa dawa za kulevya nchini.
Alisema wafanyabiashara hao wamekuwa wakiwatumia vijana kwa ajili ya kununua na kusambaza dawa za kulevya, bila ya kuzingatia athari zitokanazo na biashara hiyo haramu ambayo pia huzorotesha maendeleo ya kiuchumi kwa taifa.
Maalim Seif alieleza jhayo jana ana katika hafla ya ufunguzi wa kampeni ya kupunguza matumizi ya dawa za kulevya na athari zake shuleni, iliyofanyika Shule ya Sekondari ya Lumumba.
Alisema hatua za dharura ni lazima zitumike katika kuwashughulikia wafanyabiashara hao, vyenginevyo taifa litaendelea kuangamia kutokana na matumizi makubwa ya dawa za kulevya.
Alifahamisha kuwa wafanyabiashara wa dawa za kulevya wamekuwa wakijali zaidi maslahi yao, na kuamua kuwatumia vijana kuendeleza biashara na matumizi ya dawa hizo, jambo ambalo halikubaliki kwa mustakbali wa Zanzibar.Aliwahadharisha vijana kuwa makini na wafanyabiashara hao na kutokubali kutumiwa katika biashara hiyo. Ufunguzi wa kampeni hiyo iliyoandaliwa na “Sober Houses” chini ya ufadhili wa Hoteli ya “Double Tree Tanzania”, ulikwenda sambamba na uzinduzi wa chapisho maalum la kitabu ambacho kitatumika kufundishia shuleni.