Na: Eric Shigongo
KWANZA kabisa nimshukuru Mungu kutokana na kutupendelea kwa kuweza kuwa hai leo lakini pia kwa kuiweka nchi yetu katika amani na utulivu.
Baada ya kusema hayo leo nimeamua kuzungumzia tatizo lililojitokeza la wabunge kuporomosha matusi na nitadodosa pia demokrasia ya vyama vingi katika nchi yetu kutokana na tunachokishuhudia bungeni.
Ndani ya jengo lile lililojengwa kwa gharama kubwa za fedha za walipa kodi, waheshimiwa wamekuwa wakiporomosha matusi bila kujali kuwa wanaonwa nchi nzima, tena na watoto.
Nilitegemea kwa asilimia kubwa kwamba mfumo wa vyama vingi ungetusaidia sana kupiga hatua za maendeleo kwani tungeona chama kilicho madarakani kikisimamia yale inayoyaamini hata kama kufanya hivyo kungeliwanyima kura.
 Lakini pia tungeona vyama vya upinzani vikitofautiana na chama tawala katika misingi ya kiitikadi au kifalsafa lakini wote wakiweka kipaumbele maendeleo ya nchi.
Katika nchi ambazo demokrasia zimekomaa, wafuasi au hata viongozi wa vyama shindani huchukuliana kwanza kama ndugu wa nchi moja lakini wenye mawazo tofauti kuhusu sera na mbinu za kusukuma gurudumu la maendeleo katika jamii.
Kama hivyo ndivyo, ni wazi kwamba tusingeshuhudia matusi, kejeli au vijembe ndani ya Bunge kwani licha ya unyeti wa chombo chenyewe, walio ndani wote walishasema awali kwamba wao ni waheshimiwa!
Inajulikana kuwa katika mfumo wa vyama vingi ulioota mizizi, vyama hutumia njia za kiungwana kujiimarisha ili kushika madaraka ya dola na kutekeleza falsafa yake ya maendeleo na kamwe matusi hayawezi kusaidia kukijenga chama.
Katika siasa za demokrasia wananchi ndiyo waamuzi, ikiwa wataridhishwa na umahiri wa mawazo ya chama katika kukabili changamoto zao, hukichagua kuongoza nchi na kile kilichoshindwa hukaa pembeni kiungwana na kuimarisha ushindani bungeni huku kikijiandaa kushinda katika uchaguzi ujao.
Inapotokea hivyo wataalamu wa sayansi ya siasa husema demokrasia ya vyama vingi imeanza kukomaa.
Ni kweli kwamba wanasiasa wanapoingia katika kubadilishana madaraka kuanzia ngazi ya mtaa, udiwani, ubunge hata urais kupitia sanduku la kura ni hatua muhimu sana katika ujenzi wa utamaduni wa demokrasia ya vyama vingi.
Kitu muhimu kwa kiongozi yeyote katika nchi yetu afahamu kuwa matumizi ya madaraka yake yawe ni kwa manufaa ya kila Mtanzania.
Mfumo wa vyama vingi umekuwa ni wa demokrasia ya kushindanisha mawazo ili kupata yale bora zaidi na serikali ifanyie kazi,  sehemu muhimu ya kupima mawazo hayo ni bungeni lakini badala yake ndani ya Bunge baadhi ya waheshimiwa hao huamua kuporomosha matusi badala ya kutoa hoja.
Tunachokishuhudia sasa bungeni ni ubaguzi wa wazi kati ya wabunge wa chama fulani na kingine kwa misingi ya kisiasa na mbaya zaidi wanafikia hatua ya  kutukana hadharani. Hili Watanzania wote hawakubalianinalo kabisa.
Kusema kweli niko kinyume na wabunge wote wanaosahau matatizo ya wananchi na kwenda bungeni kutukanana. Nasema hivyo kwa sababu hii ni nchi yetu sote, maskini na matajiri.
Leo hii Mtanzania yeyote akifanya kosa adhabu yake haiwezi kuwa kumfukuza nchini kwani huko atakapopelekwa hatapokelewa. Kama hivyo ndivyo, ni jukumu la wapenda haki na maendeleo kukemea wabunge ambao ndiyo wawakilishi wetu kutumia muda wao kwa kutukanana.
Ni wajibu wetu Watanzania kuhakikisha kuwa wabunge wanajadili mambo kwa masilahi ya taifa na siyo chama fulani cha siasa kwa sababu wananchi wakisalitiwa na Bunge watakuwa wamesalitiwa na serikali.Bungeni tunashuhudia wabunge wakipingana hata kwa kitu ambacho ni cha manufaa ya taifa. Mbunge atapinga kwa sababu hoja imetolewa na mbunge kutoka chama ambacho siyo chake, hii maana yake itikadi imewekwa mbele kuliko utaifa.
Huu ni ubaguzi na vyama sasa ni kama kabila, wabunge na wananchi wanabaguana kwa masilahi yao na vyama vyao na siyo kwa taifa.
Wabunge wanaofanya hivyo wajione kuwa wako sawa na wanajeshi waliokuwa wakifanya mapinduzi kwa kupindua marais, walikuwa wakifanya hayo kwa manufaa yao.
Wote tujiulize, je, wabunge wetu hawana uimla kwa vile wanachaguliwa? Je, hawajijengi kiuchumi kwa kupiga dili za kuwaingiza wananchi katika umaskini ili wao wapate fedha za kununua uhalali wa madaraka kwa wananchi katika uchaguzi ujao wa mwaka 2015?
Kila aliyeshiriki kuchagua kiongozi katika nchi hii ajiulize  je, kiongozi wake ana ajenda ya maendeleo kwa wananchi? Mbunge wako bungeni hajajiingiza katika hili la kutukanana? Kama kajiingiza ni wazi kabisa kwamba hafai kuongoza na hakikisha harudi katika uchaguzi ujao.
Ndugu zangu, niwashauri kwamba viongozi ambao watalifikisha taifa hili katika nchi yenye asali na maziwa ni wale wenye uzalendo wa kweli, wenye moyo wa kushirikiana na viongozi wote, hasa wenye mawazo ya kuendeleza nchi bila kujali kama anayetoa wazo ni mpinzani au la.
Matusi, kejeli, vijembe ndani ya bunge haviwasaidii wapiga kura hata kidogo na badala yake vinawaudhi. Wabunge wanaofanya ‘madudu’ hayo wanajulikana na hakika wanatia aibu na kulifedhehesha bunge.
Lakini Mheshimiwa Spika naye anapaswa kulaumiwa, kwa nini mbunge anatoa tusi na huchukui hatua ili iwe fundisho?
Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli.